WATANZANIA MILIONI 31 KUPIGA KURA SERIKALI ZA MITAA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uandikishaji wapigakura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Na Nora Damian, The Page 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amesema zaidi ya Watanzania milioni 31.2 sawa na asilimia 94.83 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu. 

Idadi hiyo inatajwa kuongezeka kulinganisha na wapigakura milioni 19.6 waliojiandikisha katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019. 

Akizungumza leo Oktoba 21,2024 na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema kati ya walioandikishwa wanawake ni 16,045,559 wakati wanaume ni 15,236,772. 

“Mafanikio haya yamechagizwa na uelimishaji na uhamasishaji uliofanywa katika ngazi zote muhimu, mikoa imefanya kazi nzuri katika zoezi hili ndiyo maana kuna ongezeko la idadi ya wananchi waliojitokeza ikilinganishwa na mwaka 2019,” amesema Mchengerwa. 

Amesema orodha ya wapigakura itaanza kubandikwa kuanzia leo ili kuwawezesha wananchi kukagua majina yao na kurekebisha taarifa au kuwaondoa watu waliofariki na kwamba ukaguzi huo utahitimishwa Oktoba 27,2024. 

Waziri huyo amevitaka vyama vya siasa vihamasishe wananchi kujitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ambapo fomu zitaanza kutolewa Oktoba 26 hadi Novemba Mosi, 2024. 




Powered by Blogger.