DK. MPANGO ATAKA TAFITI ZAIDI MABADILIKO YA TABIA


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango amesema zinahitajika tafiti za kina pamoja na mikakati katika kufanya mapinduzi ya kitamaduni kubadili tabia na mazoea yasiyoyafaa yanayojitokeza katika jamii ambayo ni kikwazo kwa maendeleo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa kusherehekea miaka 30 ya Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) uliofanyika Dar es Salaam.

Ametaja baadhi ya mazoea na tabia hizo ni pamoja na kutojali muda, kutokuwa na uaminifu mahali pa kazi pamoja na kutumia njia zisizofaa katika kupata kipato.Ameitaka ESRF pamoja na Watalaam wa Fikra Tunduizi (Think Tank) kuangazia pia tabia za hivi karibuni za vijana kushiriki katika mahusiano na wanawake waliyowazidi umri maarufu (mashangazi) kama njia rahisi ya kujikimu, kutumia muda mwingi bila kufanya kazi kwa kushinda vijiweni, uchezaji kamari, utupaji taka ovyo, uchomaji moto ovyo wa nyasi na misitu pamoja na ubinafsi.

Pia amesema ni muhimu kuangazia tabia zingine kama vile matumizi makubwa ya fedha katika anasa kuliko kuweka akiba ikiwemo uchangiaji zaidi katika matukio ya sherehe na tafrija kuliko kusaidia gharama za elimu na matibabu kwa familia za kipato cha chini. 

Mengine ni kuongezeka kwa tabia ya utegemezi pamoja na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake, watoto pamoja na vitendo vya ushirikina ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa ESRF kufanya tafiti katika maeneo mengine kama vile mabadiliko ya haraka ya teknolojia, kutokuwa na uchumi stamihilivu, mizozo mikali inayopelekea mivutano ya kisiasa pamoja na kufanya tafiti kufahamu mienendo ya soko la ajira na namna vijana watakavyoweza kuendana nayo. Amesema ili kutumia vema idadi kubwa ya vijana iliyopo barani Afrika ikiwemo Tanzania, taasisi za tafiti zinapaswa kuainisha ufadhili endelevu wa miradi na programu zinazopendelewa na vijana kulingana na vipaumbele vya Taifa.

Aidha amesisitiza umuhimu wa tafiti katika sekta ya madini ikiwemo madini adimu ya kimkakati ambayo ni msingi wa viwanda vya teknolojia ya juu, tafiti juu ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwa njia endelevu pamoja na tafiti zitakazolenga kufanya mageuzi ya maeneo yanayotambulika kama nusu jangwa kuwa fursa mpya ya uzalishaji nchini.

Amesema zinahitajika tafiti za maendeleo ya kilimo kwa kutumia maji yaliyopo chini ya ardhi pamoja na uvunaji maji ili kuleta mabadiliko katika maeneo hayo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuendelea kufanya kazi na kusaidia utafiti wa kiuchumi na uchambuzi wa sera unaofanywa na ESRF pamoja na taasisi nyingine za ndani ikiwa lengo ni kuongeza ufadhili wa utafiti na uwekezaji katika miundombinu inayounga mkono tafiti hizo.




Powered by Blogger.