TARURA YAUNGANISHA VIJIJI VYA IFINSI, KAMBANGA NA BUGWE WILAYANI TANGANYIKA
Na Mwandishi Wetu, Katavi
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umekamilisha ujenzi wa vivuko na Daraja la Mto Mnyamasi lenye urefu wa mita 20 pamoja na kufungua barabara ya Kambanga - Ifinsi yenye urefu wa kilomita 37.
Barabara hiyo inaunganisha vijiji vya Ifinsi, Kambanga na Bugwe vilivyopo kata ya Tongwe Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Japhet Bengesi, ameishukuru serikali kwa kutoa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja na vivuko na kufungua barabara inayoanzia Kambanga - Ifinsi mpaka Kijiji cha Bugwe ambapo imewezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
“Kikwazo kikubwa kilikuwa katika Mto Mnyamasi ambalo ni eneo la bonde, hapo awali hakukuwa na mawasiliano lakini kutokana na juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutuletea fedha, tumeweza kujenga makalavati ya ukubwa tofauti saba na barabara unganishi ambapo imekuwa mkombozi mkubwa maana hili ni eneo kubwa la uzalishaji," amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mnyamasi, Ngisa Muyanga, ameishukuru serikali kwa kuwatengenezea barabara hiyo ambayo awali ilikuwa haipitiki, wananchi walikuwa wanavuka kwa shida kusafirisha bidhaa zao.
“Tulikuwa tunavuka kwenye maji kipindi cha masika, akina mama walikuwa wanajifungulia njiani magari yalikuwa hayapiti na tulikuwa tunashindwa kusafirisha biashara zetu, lakini kwa sasa tunaishukuru serikali, watu wanavuka kwa urahisi na magari yanapita vipindi vyote”, amesema Ngisa.
Naye Mkazi wa Kijiji cha Ifinsi, Ibrahimu Temi, amesema kipindi cha nyuma miundombinu ilikuwa tabu walikuwa wanabeba magunia yenye mazao mabegani kuvuka ng’ambo, lakini sasa magari yanaingia kijijini na wanakoboa mpunga na kusafirisha mchele na kuufikisha Mpanda kwa urahisi.
Kwa upande wake, Eunice Shola mkazi wa Kijiji cha Ifinsi, amemahukuru Rais Samia kwa kupata barabara hiyo kwani wanawake walikuwa wanapata shida kuvuka na wengine walijifungulia njiani, sasa hivi hawana shida ya usafiri magari ya wagonjwa yanafika hadi kjijini na kupeleka wananchi hospitali.
