MAFURIKO JANGWANI SASA BASI, BILIONI 97 KUJENGA DARAJA
Na Nora Damian, The Page
Wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na watumiaji wengine wa Barabara ya Morogoro wataondokana na kero ya mafuriko katika eneo la Jangwani baada ya Serikali kuanza mipango ya ujenzi wa daraja jipya litakalogharimu Sh bilioni 97.1.
Kwa muda mrefu Daraja la Jangwani limekuwa kero hasa nyakati za mvua kutokana na kujaa maji na kusababisha barabara hiyo kufungwa mara kwa mara.
Akizungumza leo Oktoba 22,2024 wakati wa kusaini makubaliano ya ujenzi wa daraja hilo litakalojengwa na Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC), Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema litajengwa kwa miaka miwili.
Amesema ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 390 utahusisha pia barabara unganishi zenye urefu wa mita 700.
Waziri huyo amesema pia Sh bilioni 125 zimetengwa kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es Salaam iliyoharibiwa na mvua za Elnino ambapo wanatarajia kujenga Daraja la Kigogo lenye urefu wa mita 50, Daraja la Mkwajuni (mita 20), JKT Ununio, daraja la Mzinga, kujenga mifereji katika Barabara ya Moroco – Mwenge – Africana – Mlalakuwa, Mbagala Rangi tatu – Vikindu na Kibada – Mwasonga ambayo tayari mkandarasi amepatikana.
Waziri Bashungwa ameelekeza pia mkandarasi anayejenga awamu ya tatu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka kutoka Gongo la mboto hadi katikati ya jiji asimamiwe ipasavyo ili afanye kazi kwa saa 24.
“Nikiwa natokea ‘airport’ nikipita huwa sioni akifanya kazi usiku wakati teknolojia inaruhusu, naelekeza asimamiwe ipasavyo na nimeshamwambia utendaji wake wa miradi ambayo anayo ndiyo utamuhakikishia kama atapata kazi tena,” amesema Bashungwa.
Waziri huyo pia amewaelekeza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kushirikiana na Kikosi cha Usalama Barabarani kupunguza foleni kwa kuruhusu njia za mwendokasi zitumike hadi mabasi yatakapokuja.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albart Chalamila, ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Daraja la Jangwani na kuiomba iendelee kulitupia jicho jiji hilo kwa kuwa barabara nyingi zimechakaa na taa za barabarani haziwaki.
