WALIOMBAKA, KUMLAWITI BINTI KWA ZAMU WAHUKUMIWA JELA MAISHA


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Washtakiwa wanne wakiwamo Askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti na mkazi wa Yombo jijini Dar es Salaam wamehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwatia hatiani.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024, waliotiwa hatiani ambao maarufu kama ‘waliotumwa na afande’ ni MT 140105 Clinton Damas maarufu kama Nyundo ambaye ni askari wa JWTZ, C.1693 Praygod Mushi ambaye ni askari Magereza, Nickson Jackson na Amin Lema maarufu Kindamba.

Hukumu hiyo imetolewa leo Septemba 30,2024 ambapo wametakiwa pia kumlipa binti huyo fidia ya Sh milioni moja kila mmoja.

Sakata hilo liliibuka mwanzoni mwa mwezi uliopita baada ya video kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo wakidai kuagizwa na afande.

Kulingana na taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Agosti 9,2024 tukio hilo lilifanyika Mei 2024 katika eneo la Swaswa jijini Dodoma.



Powered by Blogger.