SERIKALI YATAKA UDHIBITI BIDHAA BANDIA UONGEZWE SOKO HURU LA AFRIKA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dk. John Simbachawene, akizungumza wakati alipotembelea ofisi za Tume ya Ushindani (FCC), Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Serikali imeiagiza Tume ya Ushindani (FCC) kuongeza udhibiti wa bidhaa bandia ili kulinda walaji na kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika Soko Huru la Afrika.

Maagizo hayo yametolewa leo Septembaa 24,2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dk. John Simbachawene, wakati alipotembelea ofisi za FCC Dar es Salaam kujifunza na kufahamiana na watendaji wa tume hiyo.

Amesema soko hilo litakapoanza ushindani utakuwa mkubwa kwa kuwa nchi mbalimbali za Afrika zitaleta bidhaa zake hivyo, Tanzania isipokuwa makini inaweza kujikuta bidhaa zake zinakosa soko.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio, akizungumza wakati Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dk. John Simbachawene (hayupo pichani), alipotembelea ofisi za tume hiyo Dar es Salaam.

“Soko Huru la Afrika litakapoanza FCC itakuwa na kazi kubwa kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini siyo feki, itatulazimu kama nchi kuongeza udhibiti wa bidhaa ambazo haziko katika viwango. Mbali ya Bandari ya Dar es Salaam tuna njia nyingine ambazo zinatumika kupitisha bidhaa karibu nane; kuna Tunduma, Holili, Tarakea, Namanga na nyingine.

“Kama taasisi muongeze nguvu ya kuwa na maofisa wengi zaidi ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa bandia tuweze kuwalinda walaji, tujilinde sisi wenyewe na kulinda uchumi wetu,” amesema Dk. Simbachawene.

Dk. Simbachawene amesema ameridhishwa na maelezo aliyoyapata ambayo yamempa picha halisi ya kuijua tume hiyo na kuitaka iendelee kufanya kazi na kuiunga mkono Serikali ili kuinua uchumi na kuwasaidia wananchi kuwa na maisha bora.

Naye Mkurugenzi wa Tafiti, Miungano ya Makampuni na Uraghibishi katika tume hiyo, Zaytuni Kikula, amesema wamekuwa wakifanya tafiti kubaini matendo yanayoweza kuathiri ushindani na kama wakiona mapungufu wanatoa ushauri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema mwelekeo wao ni kuwa na wafanyakazi katika vituo vyote vya mpakani ili kuhakikisha bidhaa bandia haziingii au kuzalishwa nchini.

“Kuna mipaka minane na tumeanza harakati za kuwepo kote huko, kwa sasa tuko ofisi za kanda tu. Tutatumia fursa ya Soko Huru la Afrika kufanikisha mkakati huu,” amesema Erio.

Mkurugenzi huyo pia ameishukuru Serikali kwa kuridhia kupitishwa kwa marekebisho ya Sheria ya FCC ambayo ilianza kutumika tangu mwaka 2003 na kwamba wanaamini italeta ufanisi zaidi.


Powered by Blogger.