WATU 500 WAPATIWA VYETI VYA KUZALIWA MAONESHO YA NANENANE DODOMA

Wananchi wakipata huduma katika banda la Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Na Nora Damian, The Page

Zaidi ya watu 500 wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Akizungumza leo Agosti 8,2024 na Waandishi wa habari katika banda la wakala huo, Ofisa Mawasiliano wa RITA, Jafari Malema, amesema walianza kutoa huduma mbalimbali za usajili na vyeti vya kuzaliwa tangu Agosti Mosi mwaka huu na mwamko wa wananchi umekuwa mkubwa.

Amesema pia wanatoa huduma za usajili na vyeti vya vifo, usajili wa bodi za wadhamini, usajili wa ndoa na talaka, kuandika na kuhifadhi wosia, usimamizi wa mirathi na msaada wa kisheria bila malipo. 

"Huduma ambayo watu wana mwamko sana ni hii ya vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya vifo na masuala ya ndoa, huduma ya kusajili vyeti vya kuzaliwa na vifo tumeiweka kidijitali mwananchi anaweza akajisajili alipo kwa kutumia mfumo wetu wa E – Rita na akija na fomu aliyoipakua kutoka kwenye maombi yake tunampatia cheti chake ndani ya saa 24.

“Upande wa wosia wanakuja lakini si wengi ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu watu wafahamu umuhimu wa kuandika wosia kwa sababu baadhi ya watu wana mtazamo kwamba ukiandika wosia unajichulia wakati si kweli.

“Ukiandika wosia haina maana kwamba unakwenda kufa kwa sababu ziko wosia nyingi ambazo zimehifadhiwa na watu walioziandika bado wako hai, ni sehemu ya kuandaa familia yako mara baada ya kufariki wasije kugombana au kugombani mali na kusababisha migogoro,” amesema Malema.Amesema wana timu ya wataalam wa kutosha kutoka makao makuu Dodoma na Dar es Salaam ambao wameungana kwa lengo la kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo.

Mkazi wa Kisasa Dodoma, Neema Philipo amesema; "Nimekuja kufuatilia cheti cha kuzaliwa cha mtoto na tayari nimefanya maombi nasubiri kupatiwa. Tunawashukuru Rita kwa kutuletea huduma hii.

Mkazi mwingine wa Kikuyu Dodoma, Masele Martin, amesema maofisa wa Rita wamemuhudumia vizuri na tayari amepatiwa cheti cha kuzaliwa cha mdogo wake. 




Powered by Blogger.