TRA: WAKULIMA CHANGAMKIENI ZANA ZA KILIMO ZILIZOPEWA MSAMAHA WA KODI

Ofisa Msimamizi Kodi Mwandamizi wa TRA, Philipo Eliamini, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dodoma.

Na Nora Damian, The Page

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wakulima kuchangamkia fursa ya kuagiza zana za kilimo zilizopewa msamaha wa kodi ili kuongeza tija kwenye kilimo.

Akizungumza leo Agosti 2,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima maarufu Nanenane yanayofanyika Kitaifa jijini Dodoma, Ofisa Msimamizi Kodi Mwandamizi wa TRA, Philipo Eliamini, amesema serikali imeweka misamaha ya kodi katika zana mbalimbali ili kuongeza tija kwenye kilimo.

“Msamaha unaotolewa ni wa zana zinazotumika kwenye kilimo kama vile matrekta, pembejeo mbalimbali na kwa mwaka huu wa fedha (2024/2025) ‘power tillers’ zimeongezeka kwenye msamaha wa kodi. Watengenezaji wa ndani wa mafuta ya alizeti mwaka jana walipewa msamaha wa kodi na mwaka huu wameongezewa tena,” amesema Eliamini.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye alitembelea banda hilo, Profesa Riziki Shemdoe, amewashauri wakulima na watu wengine wanaoagiza zana zenye misamaha ya kodi wahakikishe wanawasilisha mapema nyaraka husika katika ofisi za TRA kurahisisha utoaji mizigo.

Aidha ameitaka TRA kuhakikisha misamaha inayokidhi vigezo inatolewa kwa wakati ili tija iliyokusudiwa hasa kumsaidia mkulima iweze kufikiwa.

Katika maonesho hayo TRA inatoa elimu kwa umma pamoja na huduma mbalimbali kama vile makadirio ya kodi, Namba ya Mlipakodi (TIN) ambayo inatolewa bure na kuwataka wananchi kufika katika banda la mamlaka hiyo kupata huduma hizo na nyingine.
“Kuna wale wanaodaiwa kodi na wanahitaji kupata namba za malipo, zinapatikana katika banda letu, tuna wasambazaji wa mashine za kielektroki za EFD na tunatoa elimu hivyo, ni wakati mzuri wa kukutana na wadau wetu mbalimbali ili kupata elimu ya masuala mbalimbali,” amesema.

Powered by Blogger.