AMANA KUKUSANYA SH BILIONI 3 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA HOSPITALI

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana.

Na Nora Damian, The Page

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana inatarajia kukusanya Sh bilioni 3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kununua vifaa tiba vikiwemo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).

Fedha hizo zitakusanywa kupitia kampeni ya ‘Rafiki wa Amana’ ambayo itahusisha matembezi ya hisani yatakayofanyika Agosti 17 mwaka huu na chakula cha hisani Agosti 31 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Bryceson Kiwelu, amesema wanalenga kujenga wodi ya mama na mtoto pamoja na ununuzi wa vifaa tiba ikiwemo vitanda vya kisasa vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Bryceson Kiwelu.

“Tunaomba michango ya wadau mbalimbali tufanikishe kuboresha huduma za watoto waliozaliwa kabla ya wakati, tushike mkono tuivushe Amana,” amesema Dk. Kiwelu.

Amesema matembezi ya hisani yataanzia ufukwe wa Coco kuelekea Karimjee kupitia Daraja la Tanzanite na kwamba anayetaka kushiriki anaweza kununua fulana kupitia namba 18852100 au kuchangia kupitia benki yoyote kwa namba 99211169807.

Powered by Blogger.