UDSM WABEBA AJENDA NISHATI SAFI, WAFANYIA UTAFITI MABAKI YA MATUNDA

Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce), Dk. Jovin Emmanuel, akionyesha nishati iliyotengenezwa kwa kutumia mabaki ya matunda kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kimebeba ajenda ya matumizi ya nishati safi kwa kutengeneza nishati inayotokana na mabaki ya matunda mbalimbali.

Nishati hiyo ambayo imetengenezwa kupitia utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce) ambacho ni sehemu ya Udsm, inalenga kupunguza uharibifu wa mazingira.

Akizungumza Julai 5,2024 Julai 6,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Mhadhiri Mwandamizi katika chuo hicho, Dk. Jovin Emmanuel, amesema kwa kushirikiana na wenzake wamefanya utafiti wa kuzalisha nishati mbadala kwa kutumia mabaki ya matunda.
“Tumetumia maganda ya mapapai, mananasi, maembe na matikiti maji. Kilichotusukuma kufanya utafiti ni kutokana na hali ilivyo ya nishati, nishati iliyozoeleka kama mafuta inaleta uchafuzi wa mazingira, ni ya gharama na upatikanaji wake ni wa kusuasua kwa sababu inatoka nje.

“Kutokana na hali hiyo kukawepo umuhimu wa kupata nishati mbadala ambayo haichafui mazingira inayoweza kuzalishwa kutoka katika vitu vya kawaida,” amesema Dk. Emmanuel.

Amesema walichukua matunda na kuyapeleka maabara kisha kufanya tafiti ambapo walipata juisi na kutengeneza mtambo wa kuichuja na kupata bidhaa yenye viwango tofauti.

Kwa mujibu wa mtafiti huyo, bidhaa walizopata kutokana na utafiti huo hazijaongezwa kemikali zozote na kwamba zinaweza kutumika kuendesha magari (asilimia 92), kupikia, kwenye maabara shuleni, spirit ya kawaida na vitakasa mikono.

“Kwa jamii kuliko kutumia mafuta ya taa wanaweza kutumia nishati hii, hiki (anamwonyesha mwandishi) ni kibatari, unatumia kidogo na ukiwasha kinatoa mwanga wa kutosha na haina moshi wala harufu. Kwenye maabara wanaonunua kemikali kutunza ‘specmen’ wanaweza kutumia nishati hii.

“Sanitizer (vitakasa mikono) vinahitajika kila siku, vinatumia spirit ambayo inatoka viwandani lakini hii inaweza kutumika kwa sababu ni rahisi na haina gharama kubwa za uzalishaji,” amesema.

Amesema wanaendelea kutafuta wabia kupata fedha za kuzalisha bidhaa hizo kwa wingi ili ziweze kuingizwa sokoni na kuwafikia wananchi kwa gharama nafuu.

Serikali imeanzisha programu ya miaka 10 ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Dk. Emmanuel amewakaribisha wananchi kutembelea katika banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika maonesho kupata elimu kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na tafiti zilizofanywa na wanataaluma kwa kushirikiana na wanafunzi.



Powered by Blogger.