EWURA YASISITIZA WANAOTAKA KUFANYA SHUGHULI ZA GESI ASILIA KUOMBA VIBALI


Na Nora Damian, The Page

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema watu wanaotaka kufanya shughuli za uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia wanapaswa kufuata utaratibu wa kisheria kwa kuomba vibali vya ujenzi ambavyo vinatolewa na mamlaka hiyo.

Mamlaka hiyo ina jukumu la kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na chini wa gesi asilia zinazojumuisha uchakataji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji wa gesi asilia nchini.

Akizungumza Julai 6,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, amesema vibali hivyo vinatolewa kupitia kifungu cha 126 cha Sheria ya Petroli.
Kaguo alikuwa akizungumza kuhusu utaratibu wa maombi ya vibali na leseni za shughuli za uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia nchini.

“Vibali vya ujenzi hutolewa ndani ya siku 30 baada ya kupokelewa kwa maombi yaliyokamilika na uhalali wa vibali ni kati ya miaka miwili hadi mitano kwa kuzingatia aina ya miundombinu inayojengwa. Miundombinu inayodhibitiwa ni pamoja na mitambo ya uchakataji, bomba la usafirishaji, usambazaji, vifaa vya kuhifadhi na mitambo ya kujaza gesi kwenye magari,” amesema Kaguo.

Kuhusu leseni za uendeshaji miundombinu ya gesi asilia amesema hutolewa ndani ya siku 60 baada ya kupokelewa maombi yaliyokamilika na uhalali wa leseni ni kati ya miaka mitano hadi 20.

Aidha amesema maombi ya vibali vya ujenzi na leseni za shughuli za gesi asilia hufanyika mtandaoni kupitia Mfumo wa Taarifa za Leseni na uagizaji (LOIS) unaopatikana katika tovuti ya EWURA.

Kulingana na EWURA ada za maombi ya vibali ni kati ya Sh milioni 5 hadi Sh milioni 20 wakati ada za leseni ni kati ya Sh milioni moja hadi Sh milioni 10.





Powered by Blogger.