EWURA YAHAMASISHA UWEKEZAJI KATIKA GESI ASILIA ILIYOBANWA

Na Nora Damian, The Page

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imewataka watu wanaotaka kuwekeza katika gesi asilia wawekeze katika vituo vya gesi asilia iliyobanwa (CNG).

Mamlaka hiyo imesema Shirika la Viwango Tanzania (TBS), tayari lilishafanya marekebisho ya viwango vya ubora ambapo kituo chochote Tanzania kinaweza kuweka mradi wa ufungaji wa mifumo ya CNG.

Akizungumza Julai 5,2024 katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) kwenye banda la mamlaka hiyo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo, amesema wanahamasisha wenye gari wayarekebishe ili watumie gesi hiyo.
"Ili CNG iweze kutumika nchi nzima itaenda kwa kusogea tofauti na bidhaa nyingine, na hilo ni wazo la wizara kwamba EWURA ichukue kama chanzo kingine cha matumizi ya nishati mbadala kutokana na hali mafuta duniani," amesema Kaguo.

Aidha amesema katika banda hilo pia kuna ripoti mbalimbali za utendaji wa sekta ya umeme, maji, petroli na ya gesi asilia.

Meneja huyo amesema katika banda hilo wataalam wote wa gesi asilia, sekta ya maji, petroli, leseni wapo na kwamba wamejipanga kuhakikisha waatatua changamoto zote za wadau.

"Kuna kina mama wamekuja wanataka kuungiwa gesi na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, tumewaelekeza waende TPDC ili waweze kuelewana na kuungiwa gesi. Hi inakuwa ni majibu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye anataka Tanzania iwe moja ya nchi bora kwenye suala la nishati safi ya kupikia," amesema.

Amesema watu wengi waliofika katika banda lao wana shauku ya kuwa na leseni ya umeme na kwamba wanatoa leseni ndogo za ukandarasi zenye madaraja mbalimbali.

Powered by Blogger.