WAZAZI WAASWA KUWAFUNDA WATOTO KUDHIBITI MMOMONYOKO WA MAADILI

Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi inayomilikiwa na Serikali ya China (CCCC) Tawi la Tanzania, wakikabidhi vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Bajeviro wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto, Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

Wazazi na walezi wametakiwa wasiwafiche watoto wao badala yake wakae nao na kuwaeleza mambo wanayotakiwa kuyaepuka waondokane na mmomonyoko wa maadili hapa nchini.

Mkuu Msaidizi wa Shule ya Awali na Msingi ya Bajeviro iliyopo wilaya ya Kinondoni, Tausi Makemba, amezungumza hayo wakati wakiadhimisha Siku ya mtoto wa Afrika na kupokea vifaa vya shule yakiwemo mabegi na madaftari waliokuwa wanakabidhiwa wanafunzi 100 wanaoishi mazingira magumu kutoka Kampuni ya ujenzi inayomilikiwa na Serikali ya China (CCCC) Tawi la Tanzania.

Mahemba amesema mzazi au mlezi anatakiwa awaeleze mambo ambayo wanatakiwa kuyafanya ili waweze kujua haki zao za msingi ili waepukane na mambo ambayo hawatakiwi kuyafanya kwenye jamii.

Amesema mtoto anapoelezwa ukweli bila kufichwa atawajibika kwa mzazi au mlezi na jamii kwa ujumla kwa kuwaheshimu, kusoma kwa bidii na kuepukana na vishawishi vya mtaani ikiwemo uhalifu, uvutaji wa dawa za kulevya zinazosababisha kupoteza ndoto zao za baadaye.

"Mtoto akijua haki zake za msingi na wajibu wake kupitia elimu katika malezi ya nyumbani kama anaishi na mzazi au mlezi itamsaidia kwa kuwa sasa hivi kuna unyanyasaji mwingi ambao unavunja sheria na haki za mtoto hasa kupitia jamii inayomzunguuka," amesema Mahemba.
Naibu Mkurugenzi wa Kampnuni ya CCCC Tawi la Tanzania, Yue Guozhu, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto, Dar es Salaam.

Amesema walimu wanakaa na wanafunzi kwa saa nane na kupitia somo la uraia na maadili wanawafundisha jinsi ya kuishi na kuwaelekeza haki zao za msingi wanazostahili kuzipata.

Mahemba ameishukuru kampuni hiyo Kwa kuungana shule hiyo katika kusherehekea siku ya mtoto wa Afrika Duniani Kwa kutoa vifaa mbalimbali vya shule kwa watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi A, Steven Kinyota, amesema watoto hawapewi haki zao za msingi ambapi mzazi anaweza kuondoka kazini na kumuacha mtoto anajichunga mwenyewe na anaporudi hana muda wa kumuuliza mwanawe alivyoshinda.

"Matokeo yake watoto wa siku hizi hawana heshima kwa wazazi wao pamoja na jamii inayomzunguka wakimuona mtu mzima hawampokei mzigo wakati mwingine hawamtii kwa kuwa mzazi wake hajakaa naye na kumueleza haki zake za msingi ikiwemo uwajibikaji kwenye jamii," amesema Kinyota.

Kwa upande wa mwanafunzi wa shule hiyo, Nayfat Malik, amesema vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Serikali ya China vitawasaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu kujifunza kwa weledi

Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya CCCC Tawi la Tanzania, Yue Guozhu amesema wanatambua umuhimu wa siku hiyo ndiyo maana waliamua kusherehekea na wanafunzi wa shule hiyo .

Guozhu amesema kampuni hiyo ambayo inafanya kazi za ujenzi katika miradi mbalimbali nchini imekuwa pia ikirudisha sehemu ya faida wanayopata kwenye jamii kama vile kutoa misaada ya vifaa vya kujifunzia katika shule.

Kila mwaka Juni 16 Tanzania inaungana na nchi zingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

Chimbuko la maadhimisho haya ni azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini waliouawa Juni 16,1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Powered by Blogger.