MAGANZA AAHIDI KUIJENGA UPYA TLP
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Mhandisi Aivan Maganza, akizungumza baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Dar es Salaam.
Na Nora Damian, The Page
Mwenyekiti mpya wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Mhandisi Aivan Maganza amesema amejipanga kukijenga upya chama hicho akitaka apewe miezi mitatu.
Maganza ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa chama hicho, amechaguliwa leo Juni 29,2024 baada ya kupata kura 33 katika uchaguzi uliofanyika Dar es Salaam.
Akizungumza na wajumbe wa chama hicho amesema ataunda upya sekretarieti ya chama hicho na kutoa onyo wenye nia ya kukivuruga chama waanze kuondoka.
"Niliweka nadhiri mbele ya marehemu Mzee Mrema (aliyekuwa Mwenyekiti) nilisema sitatoka TLP kama chama hakijawa kikubwa Tanzania. Kwahiyo nawahakikishia chama kinakwenda kujengwa upya, tutakwenda mikoa yote, chama kinaenda kuendeshwa kisomi.
"Tunakwenda kubadilisha jengo la makao makuu lisikae na kuwa kichefuchefu, wale ambao wako kwa nia ya kukwamisha chama kuanzia sasa waondoke, nataka nibaki na watu wanaoweza kufanya kazi.
"Nataka chama kijulikane mtaani, vijijini, mijini na mitandaoni...nipeni miezi mitatu nitakuja kutoa ripoti," amesema Maganza.
Mwenyekiti huyo pia amemteua Riziki Gaga kuwa Katibu Mkuu mpya.
Makamu Mwenyekiti wa TLP Bara, Dominata Rwechungura, amewapongeza wanachama kwa kuwa wavumilivu na kuhakikisha maamuzi ya halmashauri kuu ya kumtafuta mwenyekiti taifa yanakamilika.

