DOYO AJITOSA UENYEKITI ADC AKIAHIDI KUKIBADILISHA KIWE CHAMA SHINDANI
Aliyekuwa Katibu Mkuu Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Na Nora Damian, The Page
Vuguvugu la uchaguzi wa ndani ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) limeanza kupamba moto baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Doyo Hassan Doyo kutangaza kuwania nafasi ya uenyekiti.
Doyo ametangaza uamuzi huo leo Juni 6,2024 wakati na mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam.
Chama hicho kilisajiliwa rasmi Agosti 2012 ambapo Said Miraji alikuwa Mwenyekiti wa kwanza na kufuatiwa na Hamad Rashid Mohamed aliyeng’atuka hivi karibuni.
“Nimekaa na Hamad Rashid miaka 10 katika utendaji na hatujakwaruzana au kufokeana hivyo, nina Adamu na nidhamu katika kuendesha chama.
“Malengo na madhumuni yangu ni kutengeneza chama mbadala, nitakibadilisha ADC kiwe chama cha ushindani,” amesema Doyo.
Doyo ambaye amesema atachukua fomu Juni 11,2024 amewaasa wanachama wengine wa chama hicho kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali ili kuwe na ushindani sawa.
“Sijakataza wengine kuja kuomba nafasi ya uenyekiti wa chama, tunataka tuwe wagombea wengi hakuna tatizo lolote…nimejipanga vya kutosha,” amesema.

