SERIKALI YAPIGIA CHAPUO BUNIFU ZINAZOJIBU CHANGAMOTO ZA WATANZANIA

Meneja Mradi wa Funguo unaowezesha wabunifu wachanga, Joseph Manirakiza, akizungumza wakati wa kongamano lililokuwa likijadili mchango wa vyombo vya habari kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania.

Na Nora Damian, The Page

Wakati Tanzania ikisherehekea maadhimisho ya 10 ya Wiki ya Ubunifu, Serikali imeeleza juhudi zinazofanywa kukuza sekta hiyo huku ikihamasisha kuwapo kwa teknolojia zinazotoa majibu ya changamoto za wananchi.

Akizungumza leo Mei 20,2024 Mkurugenzi wa Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladslaus Mnyone, amesema ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu na nyingine.

Profesa Mnyone ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, alikuwa akizungumza wakati wa kongamano lililokuwa likijadili mchango wa vyombo vya habari kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania yenye kaulimbiu ‘Ubunifu kwa uchumi shindani’.

Ametaja juhudi kadhaa zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo kutunga sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, maboresho ya mitaala ya elimu, kuanzisha vituo vya umahiri katika utafiti na ubunifu, kuandaa mkakati wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utoaji wa elimu na nyingine.

Aidha amesema serikali imekamilisha rasimu ya mkakati wa matumizi ya Tehama ili kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utoaji wa elimu.

“Ushirikishwaji na ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi unazidi kuimarika lakini ni vizuri uanzie mwanzo kwenye hatua ya utatuzi wa changamoto ndipo uelewa unakuwa mpana,” amesema Profesa Mnyone.

Akichangia mada katika kongamano hilo Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi, Bakari Machumu, amesema vyombo vya habari bado havijafanya vya kutosha katika kukuza sekta ya ubunifu na kushauri serikali ishirikishe wadau wote inapokuwa inatengeneza mikakati mbalimbali.

“Kama kunakosekana taarifa pengine hakuna uelewa wa kutosha, vyombo vya habari au waandishi wa habari wasichukuliwe kama ni magwiji au wana uelewa wa kila kitu, wanatakiwa kujengewa uwezo,” amesema Machumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Amos Nungu, amesema maboresho ya mtaala yatasaidia wabunifu kupata msingi mzuri wa kuendeleza bunifu zao.
“Serikali imekuwa ikiwasaidia wabunifu mbalimbali kuendeleza bunifu zao, fedha siyo tatizo ndiyo maana serikali imeweka mazingira wezeshi ya kuendelea kuelimisha vijana. Mtaala mpya utasaidia vijana kuwa na ujuzi na kujiamini katika kufanya bunifu zao,” amesema Dk. Nungu.

Meneja Mradi wa Funguo unaowezesha wabunifu wachanga, Joseph Manirakiza, amesema kunahitajika mjadala zaidi kuhusu dhana nzima ya ubunifu ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa kutosha.



Powered by Blogger.