4R ZA RAIS SAMIA ZITAKAVYOENZI MUUNGANO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiwapungia wananchi katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Na Nora Damian, The Page

APRILI 26 mwaka huu Tanzania iliadhimisha miaka 60 ya Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa kuungana mwaka 1964.

Mkataba wa muungano ulitiwa Saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume Aprili 22,1964 huko Zanzibar na kuthitibishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Aprili 16,1964.

Aprili 27,1964 viongozi wa chi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kubadilishana hati za muungano na Oktoba 28,1964 jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likazaliwa rasmi.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile mahusiano ya karibu na ya kihistoria, undugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya kisiasa baina ya vyama vya TANU na ASP.

Ni baraka kwa taifa kufikia umri huo kwa sababu yako mataifa yaliyojaribu kuungana lakini hayakufanikiwa na mengine yaliungana lakini muungano haukudumu hivyo, muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa tofauti na kudumu kwa zaidi ya nusu karne.

Katika kipindi cha miaka 60 taifa limepiga hatua katika mambo mbalimbali kama vile ya huduma za kijamii yaani elimu, afya, maji, barabara, umeme na ustawi wa jamii na kuhakikisha usalama wa wananchi na chakula.

Kazi kubwa imefanyika katika kutatua kero za muungano tangu mwaka 2006 ambapo 22 zimetatuliwa kati ya 25.

Akihutubia kilele cha sherehe za miaka 60 ya muungano, Rais Samia Suluhu Hassan, anasema ili muungano uendelee kudumu Watanzania hawana budi kuitekeleza falsafa ya maridhiano, kuvumiliana, mageuzi na kujenga nchi.

Anasema kutekelezwa kwa falsafa hizo kutajenga amani na utulivu wa kudumu nchini na kuleta maendeleo endelevu. 

“Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume wamejenga taifa huru, madhubuti na lenye matumaini hivyo, zawadi pekee wanayopaswa kupewa ni kuendelea kuudumisha muungano na kuyaenzi maono yao.

“Kwa msemo wa siku hizi tunasema tuwape maua yao, Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia muungano huu kwa sababu kwa miaka 60 tumeweza kulilinda taifa na kudumisha amani na utulivu. 

“Tumejenga umoja na mshikamano wa kitaifa, tumeimarisha undugu na tumepiga hatua kubwa za maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na kudumisha mila na desturi zetu.

“Nawasihi ndugu zangu Watanzania katika kuuendeleza muungano wetu hatuna budi kuitekeleza falsafa yetu ya maridhiano, kuvumiliana, mageuzi na kujenga nchi yetu…haya ndiyo yataendelea kutujengea amani na utulivu wa kudumu nchini na kuleta maendeleo endelevu,” anasema Rais Samia.

4R ndiyo mwelekeo wa Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipokabidhiwa kijiti Machi 2021 ambapo amekuwa akisisitiza dhamira yake ya kuijenga Tanzania moja yenye ustawi kwa wananchi wote.

Mara zote wito wake umekuwa kutaka kujenga jamii yenye maelewano, umoja na mshikamano, uzalendo, maridhiano, ustahamilivu na yenye uchumi unaokua kwa wote.

“Tutajitahidi kufanya mabadiliko katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi na katika sheria za uchaguzi ili Tanzania iende na wakati na kutoa fursa zaidi kwa watu wengi kunufaika kiuchumi.

“Tutajitahidi kuijenga Tanzania yenye haki, demokrasia na usawa na mafanikio na ndiyo maana katika kipindi hiki tulikuja na ‘idea’ nne (akimaanisha maridhiano, ustahamilivu, mabadiliko na kujenga upya)…vyama vya siasa tunazungumza, tunaelewana,” anasema Rais Samia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa Sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Hatua mbalimbali zimechukuliwa na Rais Samia katika kuimarisha demokrasia na utawala bora tangu aingie madarakani ambapo ameshuhudiwa akifungua ukurasa mpya wa siasa na demokrasia lakini kubwa ni fursa ya maridhiano ambayo yanaendelea mpaka sasa.

Amekutana na vyama vya siasa, mtu mmoja mmoja na wadau mbalimbali wa demokrasia huku akiruhusu kufanyika kwa mikutano ya kisiasa ya hadhara ambayo ilipigwa marufuku tangu mwaka 2016.

Rais Samia pia alitangaza nia yake ya kuhakikisha Tanzania inachangamana na jumuiya ya kimataifa na kuihakikishia dunia kuwa Tanzania haitajifungia, itayapa kipaumbele mashirikiano ya kiuchumi na kimaendeleo.

Aidha chini ya utawala wake Rais Samia alielekeza kupitiwa mienendo ya baadhi ya kesi nchini pamoja sheria zilizoonekana kuwa na ukakasi na kuzifanyia marekebisho hatua iliyowezesha watu zaidi ya 400 waliokuwa mahabusu kwa kesi zisizo na ushahidi kuachiwa huru wakiwamo viongozi wa Uamsho waliokaa mahabusu kwa miaka minane wakituhumiwa kwa ugaidi.

Rais Samia anatoa wito kwa Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi ili kukuza tija kwa taifa kwani nchi imefikia uchumi wa kati ngazi ya chini na tathmini zinaonyesha kuna mwelekeo mzuri wa kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu na kuwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani ili kujenga uchumi na kuleta ustawi zaidi wa wananchi.

RAIS MWINYI

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, anasema hatua ya waasisi kuwaunganisha Watanzania ilikuwa na dhamira ya kuimarisha undugu hivyo, taifa lina wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maendeleo makubwa ambayo imeyapata katika sekta mbalimbali. 

Anasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupata sifa na heshima kubwa kimataifa kutokana na kudumu kwa muungano huku kukiwa na amani, umoja na mshikamano.

“Tutaendelea kuwa waumini wa dhati wa muungano wetu na tutahakikisha unadumu na unazidi kuimarika kwa faida ya kizazi cha sasa na wale watakaokuja baadaye,” anasema Dk. Mwinyi.

MARAIS COMORO, BURUNDI 

Rais wa Comoro, Azali Assoumani, anasema muungano umejenga misingi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuwapongeza waasisi kwa maono yao.

“Tanzania ni nchi ya mfano kwa amani, maendeleo na demokrasia. Sifa moja kubwa naweza kuitoa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watawala wote wamekuwa na ushirikiano wa karibu na Comoro.

“Tanzania imekuwa ni mwenyeji wa vuguvugu la kutafuta uhuru wa nchi zetu barani Afrika ikiwemo nchi yangu, viongozi waliotutangulia wamejenga misingi ya kukaribisha nchi zetu kuwa na ushirikiano wa karibu…ninaahidi kuendeleza na kudumisha ushirikiano uliopo,” anasema Assoumani.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, anasema Muungano wa Tanzania ni wa jumuiya hiyo kwa kuwa wananchi wote ni wamoja. 

Vijana wa sasa wanalo deni kwa Watanzania kuhakikisha wanaulinda na kuutetea muungano uendelee kudumu kwa faida ya vizazi vijavyo kwa kuendelea kufanya mazuri.

Powered by Blogger.