WAKURUGENZI MAMLAKA ZA MAJI WAPIMWE KWA KUZUIA UPOTEVU WA MAJI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema suala la upotevu wa maji lifanyiwe kazi zaidi kwa sababu linaongeza gharama za uendeshaji na kutaka wakurugenzi wa mamlaka za maji wapimwe kwa hatua wanazochukua kuzuia upotevu.
Ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa mapitio ya sekta ya maji 2024 jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji, Profesa Kitila amesema lengo kubwa la Serikali ni kukuza uchumi shindani na kuleta maendeleo ya watu na huduma ya maji ni moja ya jambo muhimu katika kufanikisha hatua hiyo hapa nchini.
“Watendaji wa sekta ya maji wanafanya kazi kubwa na nzuri, tena usiku na mchana kwa ajili ya wananchi. Waziri wa Maji halali akipambania masuala ya maji kufika katika makazi ya wananchi," amesema Profesa Kitila.
Amesema hali ya upatikanaji wa maji imezidi kuongezeka mjini na vijijini na kwa kasi ilivyo malengo yaliyowekwa na serikali yatafikiwa asilimia 85 vijijini na 95 mijini.
Amesema takwimu za hali ya upatikanaji wa maji inatokana na uwekezaji unaofanywa na serikali katika kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.
Pia amepongeza kazi ya utunzaji na uendelezaji wa vyanzo vya maji hatua ambayo moja ya matunda yake ni kujaa mapema kwa maji katika bwawa la kufua nishati ya umeme la Nyerere kabla ya muda uliokisiwa.
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF), Haji Nandule, amekabidhi hundi ya Sh milioni 800 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda baada ya kuwa ya kwanza kukidhi vigezo vya mkopo nafuu unaotolewa kwa ushirikiano na Benki ya Uwekezaji (TIB).
NWF inatoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji hapa nchini na imefungua dirisha la mikopo ya masharti nafuu kwa kushirikiana na Benki ya TIB hatua ambayo inayofanikisha huduma ya miradi ya maji kwa jamii kupitia mamlaka za maji.
NWF inatoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji hapa nchini na imefungua dirisha la mikopo ya masharti nafuu kwa kushirikiana na Benki ya TIB hatua ambayo inayofanikisha huduma ya miradi ya maji kwa jamii kupitia mamlaka za maji.

