MAKAMBA: TANZANIA IMENG’ARA KIDIPLOMASIA MIAKA MITATU YA RAIS SAMIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine, mashirika ya kikanda na kimataifa umekuzwa katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kutengeneza fursa nyingi.
Akizungumza leo Machi 20,2024 na Waandishi wa habari Makamba amesema ushawishi wa Tanzania kidiplomasia umeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia.
Amesema kiwango cha uwekezaji ulioingia nchini kimeongezeka kutoka Dola bilioni 1.03 mwaka 2020 hadi kufikia Dola bilioni 5.6 mwaka 2023.
“Katika nyanja ya diplomasia jambo kubwa ambalo nchi hulitafuta ni kuongeza ushawishi ili ipate misaada, mikopo na wawekezaji waje. Aina na idadi ya wageni waliotembelea Tanzania, mialiko na mikutano ambayo Rais Samia amealikwa na kushiriki ni mingi.
“Ukiona kiongozi (Rais Samia) sauti yake inatafutwa kwenye mambo muhimu ujue ana ushawishi yeye mwenyewe na nchi yake ina ushawishi, hii ni ishara kwamba diplomasia na ushawishi wa Tanzania umeongezeka kwa kiasi kikubwa,” amesema Makamba.
Mwenyekiti wa Kamati ya kupitia majukumu na maboresho ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk. Salim Ahmed Salim, Balozi Khamis Kagasheki, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, Dar es Salaam.
Waziri huyo amesema jitihada hizo za kuvutia wawekezaji zimetokana na sera za kiuchumi na ushawishi wa kidiplomasia uliofanywa na Rais Samia hasa katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.
“Kazi yetu imekuwa rahisi kwa sababu mwanadiplomasia namba moja (Rais Samia) ameirahisisha, tumepata misaada mikopo…mikutano, mialiko imekuwa mingi,” amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba amesema watahakikisha Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk. Salim Ahmed Salim kinaendelea kuimarishwa ili kupata wanadiplomasia nguli.
Akizungumza wakati wa kuzindua kamati ya kupitia majukumu na maboresho ya kituo hicho amesema wamejipanga kuendeleza kituo hicho kulingana na mazingira mapya ya siasa za kimataifa.
“Nchi ina hazina ya wanadiplomasia na wataalam wanaoweza kufanya kazi hiyo kwa umahiri zaidi ndiyo maana imeundwa kamati hii. Tuna uhakika kazi hii itakwenda vizuri,” amesema Makamba.
Kwa mujibu wa Makamba kamati hiyo itakayofanya kazi kwa miezi mitatu ina jukumu la kupendekeza muundo halali wa kisheria wa kituo hicho, aina ya mafunzo na mitaala inayoendana na mazingira ya sasa na namna kitakavyoweza kushirikiana na taasisi mbalimbali za aina hiyo duniani.
Majukumu mengine ni kupendekeza muundo mpya wa kituo na utaratibu wa ajira za watumishi kulingana na mahitaji ya sasa, kupendekeza na kushauri masuala ya kifedha na miundombinu inayohitajika.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Khamis Kagasheki, amesema watafanya kazi kwa weledi kuhakikisha kituo hicho kinarudi katika hadhi yake na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

