MAKAMBA ATAJA MAENEO MATANO USHIRIKIANO HUNGARY NA TANZANIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano yaliyofikiwa baina ya Tanzania na Hungary.

Na Nora Damian, The Page

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameyataja maeneo matano ambayo Hungary imekubaliana kushirikiana na Tanzania.
 
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Machi 28,2024 baina ya Waziri Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Peter Szijjarto, ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi.
 
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na masuala ya biashara ambapo kutafanyika makongamano ya biashara, ziara za kibiashara kati ya sekta binafsi ya Tanzania na Hungary na kukuza sekta ya utalii.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Peter Szijjarto, wakisaini makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi hizo.

 “Tutasaini mkataba wa usafiri wa anga kuwezesha ndege zisafiri moja kwa moja kutoka Hungary kuwezesha wataliii kuja wengi zaidi. Mwaka jana watalii kutoka Hungary walikuwa 11,000 hivyo kuna fursa zaidi ya kuongezeka kama kutakuwa na usafiri wa moja kwa moja wa anga,” amesema Makamba.
 
Maeneo mengine waliyokubaliana ni ushirikiano katika elimu kwa nchi hiyo kuendelea kufadhili vijana wa Kitanzania na ushirikiano katika sekta ya maji kwa kuwa nchi hiyo inaongoza duniani katika teknolojia ya kudhibiti maji.
 
Kwa mujibu wa Makamba, kwa miaka mingi nchi hiyo imekuwa ikitoa ufadhili wa Watanzania ambapo tangu mwaka 2018 vijana 146 wamenufaika.
 
Aidha mwaka 2023 Rais wa Hungary alipotembelea Tanzania yalifanyika makubaliano ya kutoa ufadhili wa vijana 30 kwenda kusoma nchini humo kila mwaka huku Tanzania nayo ikitoa ufadhili wa vijana watano kuja kusoma nchini.


Vilevile Hungary itawekeza katika kiwanda cha kuunganisha ndege ndogo kitakachojengwa Morogoro ili zitengenezwe nchini.
 
Katika makubaliano hayo pia Chuo cha Diplomasia Hungary kitashirikiana na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk. Salim Ahmed Salim kukuza diplomasia baina ya mataifa hayo.
 
Waziri Szijjarto ameitembelea Tanzania ikiwa imepita miaka 37 tangu Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo alipotembelea nchini.
 
Julai mwaka huu Hungary inatarajiwa kuchukua Urais wa Umoja wa Ulaya kwa miezi sita na imepanga kuendeleza ushirikiano na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).


 






Powered by Blogger.