UWEKEZAJI WA MILIONI 500 LIVERPOOL WAING’ARISHA KOROGWE

Mwonekano wa Mgahawa wa Liverpool uliopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.


Na Nora Damian, Tanga

Mwonekano wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga umeendelea kubadilika kutokana na uwekezaji mbalimbali uliofanywa ukiwemo wa Mgahawa wa Riverpool.

Mgahawa huo uliopo katika eneo la Mombo ulianzishwa mwaka 1993 na tangu wakati huo umekuwa ukihudumia wasafiri mbalimbali kutoka ndani na nje.

Akizungumza Februari 18,2024 na waandishi wa habari Meneja wa Mgahawa wa Liverpool, Salim Abdallah, amesema wamefanya maboresho makubwa ambapo pia wametenga sehemu ya kukaa watu mashuhuri (VIP).


Meneja wa Mgahawa wa Liverpool, Salim Abdallah, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma zinazotolewa na mgahawa huo.

“Tunalisha wasafiri wanaosafiri kwenda mikoani nchi jirani kwa saa 24, tunahakikisha abiria wote wanaofika katika mgahawa wetu wanapata chakula, bei zetu ni rafiki haziwaumizi Watanzania kwa sababu tunajua wako wengine ambao wana vipato vidogo,” amesema Abdallah.

Amesema kwa sasa wafanyakazi zaidi ya 30 wameajiriwa katika mgahawa huo na kuahidi kutoa huduma bora zaidi.

“Vyakula vyetu ni salama kwa sababu tunazingatia kanuni za afya, vyoo ni visafi wakati wote na vipo vya kutosha hata mabasi matano yakiingia kwa wakati mmoja tunaweza kuyahudumia…tumeweka lami ili wakati wa mvua wasafiri wasipate adha ya kukanyaga tope,” amesema.

Mbali ya vyakula pembezoni mwa hoteli hiyo kunauzwa matunda mbalimbali yakiwamo machungwa na matunda damu ambayo yanapatikana kwa wingi mkoani Tanga.

Mmoja wa madereva aliyekuwa akielekea mkoani Kilimanjaro, Andrea Emmanuel, amesema mara kwa mara amekuwa akipeleka abiria katika mgahawa huo kutokana na ubora wa huduma.

“Wakati mwingine unaweza kupeleka abiria hotelini lakini baadaye ukaambulia lawama na matusi kutokana na huduma mbovu au mazingira yasiyoridhisha hasa ya vyoo, lakini kwa Liverpool hatujawahi kupata malalamiko,” amesema Emmanuel.

Meneja wa Liverpool amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini hatua iliyovutia wawekezaji katika sekta mbalimbali.

Mara kwa mara Rais Samia amekaririwa na vyombo vya habari akisema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji kwani Tanzania ni salama na ina eneo bora la kuwekeza kutokana na kuwa na vivutio vingi vya utalii.







Powered by Blogger.