ROSTAM AANGUA KILIO NYUMBANI KWA LOWASSA

Mfanyabiashara Rostam Aziz (kushoto) akijifuta machozi baada ya kutoka kutoa pole kwa familia ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kijijini kwake Ngarash Monduli mkoani Arusha. Katikati ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Taifa Group, Absalom Kibanda.

Na Nora Damian, Monduli

Mfanyabiashara Rostam Aziz ameshindwa kujizuia na kuangua kilio baada ya kufika nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Lowassa kutoa pole.

Rostam aliyewasili kijijini Ngarash Wilaya ya Monduli mkoani Arusha leo Februari 16,2024 saa mchana alikwenda kutoa pole kwa familia lakini wakati anatoka alionekana akijifuta machozi.

Rostam anatajwa kuwa rafiki wa karibu wa kiongozi huyo, mwaka 1995 alikuwa miongoni mwa waliomshawishi Lowassa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kuwania urais. Kikwete na Lowassa walitia nia ya urais lakini walishindwa katika mchakato wa ndani ya chama.

Kikwete pia alieleza jinsi yeye na Lowassa walivyoanza safari ya urais mwaka 1995.

"Siku moja nikiwa nyumbani nikapokea ugeni, mtoto akaja chumbani akaniambia baba kuna wageni, nikaenda nikakuta marafiki zangu watatu. Kaka yangu Samuel Sitta (aliyewahi kuwa Spika wa Bunge), Edward Lowassa na Rostam Aziz.

Mfanyabiashara Rostam Aziz (katikati) akimpa pole Fredrick Lowassa ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kijijini Ngarash Monduli mkoani Arusha.

“Msemaji alikuwa Samuel Sitta, wakaja kuniambia kwamba tunataka muende na Edward Dodoma mkachukue fomu ya kugombea urais mwaka 1995. Mimi nikasema jambo hilo halipo kwenye mawazo yangu, lakini mwenzangu yeye lipo kwenye mawazo yake basi muacheni aende…yeye akasema siendi bila wewe.

“Tulibishana mpaka tukafika mahali tukakubaliana basi acha twende, mchakato wa ndani ya chama mwenzangu hakubahatika, mimi nikabahatika kuwemo katika wale watano.

“Baadaye tukapiga kura kwenye NEC nikawemo katika wale watatu, kwenye mkutano mkuu nikawemo katika wawili lakini kura zangu hazikutosha akapata Mzee Mkapa,” amesema Kikwete.

Amesema Lowassa ametoa mchango mkubwa katika taifa na kwamba yalitokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti mema na mazuri aliyoyafanya.

“Mwezangu aliteuliwa kuwa waziri mkuu, akapata changamoto ikabidi akae pembeni, tuliendelea kuwa pamoja, kuwa marafiki tukishirikiana kwa kila linalowezekana.

“Ninachoshauri tuendelee kumuombea kwa mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake, ametoa mchango mkubwa katika taifa, yalitokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti mema na mazuri aliyoyafanya taifa letu,” amesema Kikwete. 

Lowassa ambaye alitumikia Serikali kwa miaka 35 katika nafasi mbalimbali alifariki Februari 10,2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Februari 17,2024 nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha.

Powered by Blogger.