DK. KIJAJI ATAKA UADILIFU KATIKA SHERIA KULINDA WALAJI, WAZALISHAJI

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani duniani yaliyofanyika Dar es Salaam.

Na Nora Damian, Dar es Salaam

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji amesisitiza uadilifu katika usimamizi wa sheria pamoja na kanuni zake ili kuepuka maumivu kwa mlaji na kuumiza wazalishaji ambao wanaonekana dhaifu kwenye soko.

Amesema Sheria ya Ushindani ina umuhimu mkubwa katika kujenga uchumi wa taifa hivyo watu wakifanya biashara kwa kuizingatia watapata faida kubwa na kushindana katika masoko ya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza Desemba 5,2023 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani duniani amesema ni lazima wote waliopewa dhamana ya kusimamia sheria watambue kwamba wana dhima kubwa waliyoaminiwa na kukabidhiwa hivyo waisimamie kwa uadilifu mkubwa.

“Lengo la Serikali kusimamia uchumi wa soko si kukataza biashara bali inataka ifanyike kwa kuzingata sheria na misingi ya ushindani.

“Sisi ni wawezeshaji wa biashara, tunataka mfanikiwe ili tutengeneze ajira za vijana wetu na tuweze kupata kodi ambayo ndiyo inaendesha shughuli za kila siku za taifa letu,” amesema Dk. Kijaji.

Mwenyekiti wa FCC, Dk. Aggrey Mlimuka, akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani yaliyofanyika Dar es Salaam.

Amesema taasisi zote za biashara zinapaswa kufahamu kuwa wao ni wawezeshaji na kuendelea kuwawezesha wafanyabiashara ili kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Tume ya Ushindani na vyombo vingine vinavyosimamia masuala ya biashara viendelee kutekeleza wajibu wao wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuepuka uvunjwaji wa sheria. Kukosekana kwa ushindani katika soko hudumaza ukuaji wa uchumi kwani wawekezaji wengi hawatavutiwa kuja kuwekeza,” amesema.

Aidha amesema Rais Samia amefungua fursa nyingi zenye kujenga uchumi imara na zenye kuhimili ushindani kitaifa na kimataifa na kufikia lengo la maisha bora kwa wananchi wote hivyo washindani wanatakiwa kushindana kwa uhuru na amani na si kula njama za kukwepa kushindana sokoni.

Mwenyekiti wa FCC, Dk. Aggrey Mlimuka, amesema sera nzuri zinazovutia uwekezaji zimeiwezesha tume kuendelea kupokea maombi ya kuunganisha makampuni ambapo mwaka huu wamepokea maombi 28 yenye thamani ya Sh bilioni 699.24.

“Tumepokea maelekezo tutayatekeleza ili tufanye vizuri zaidi, sisi tupo kuwezesha na si kukwamisha, hatuko hapa kuwa kikwazo,” amesema Dk. Mlimuka.

Mkurugenzi wa FCC, William Erio, amesema wametumia maadhimisho hayo kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na semina mbalimbali katika kanda zake kwa lengo la kuwajengea uelewa wadau wake.

Mkurugenzi wa FCC, William Erio, akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani yaliyofanyika Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Erio, walionufaika na mafunzo hayo ni wachimbaji madini (Kanda ya Ziwa), wazalishaji na wasambazaji wa mbegu za maua (Kanda ya Kaskazini), wakamuaji wa mchuzi wa zabibu na mafuta ya alizeti (Kanda ya Kati), wafanyabiashara na wenye viwanda (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini) na wakulima wa korosho (Kanda ya Mashariki).

“Tumepata fursa ya kutoa elimu juu ya majukumu ya FCC hususan masuala ya ushindani ikiwa ni pamoja na mambo yanayokatazwa na sheria ya ushindani na namna ambavyo njama baina ya washindani zinavyoathiri masilahi na ustawi wa jamii,” amesema Erio.

Siku ya Ushindani huadhimishwa kila Desemba 5 ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Aprili 1980 ambalo lilipitisha taratibu na kanuni za kudhibiti vitendo vinavyofifisha ushindani katika biashara ulimwenguni.









Powered by Blogger.