BRELA IONGEZE JITIHADA KUWAFIKIA WAFANYABIASHARA - CHALAMILA

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, akikata utepe wakati wa kufungua Maonesho ya Huduma za Brela na Wadau Wake yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City, Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa.

Na Nora Damian, Dar es Salaam

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) umetakiwa kuongeza jitihada za kuwafikia wafanyabiashara walipo ili kukuza sekta ya uchumi katika Mkoa wa Dar es Salaam na taifa.

Akizungumza Oktoba 24,2023 Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, amesema Jiji la Dar es Salaam lina wafanyabiashara wengi wakubwa, wa kati na wadogo na Serikali inalenga kuwakuza kwa kuhakikisha wanarasimishwa.

Komba alikuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albart Chalamila, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Huduma za Brela na Wadau Wake yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City.

“Maonesho haya yatumike kufanya tathmini, wadau wanaitazamaje Brela, wana maoni gani, kitu gani kiboreshwe zaidi. Endeleeni kuja na maboresho mbalimbali na kuwasadia wajasiriamali ambao wamesajili biashara zao kwa kulinda ‘brand’ zao,” amesema Komba.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Alama za Biashara na Huduma (IP), Seka Kasera, akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa kwenye Maonesho ya Huduma za Brela na Wadau Wake yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City, Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa.

Aidha ameutaka wakala huo kuendelea kutoa elimu kwa umma ili uondokane na vishoka ambao wamekuwa wakisababisha wananchi waone kupata huduma Brela ni gharama hasa katika usajili wa kampuni na majina ya biashara.

Komba pia amemwelekeza Ofisa Tarafa wa Kibamba, Beatrice Mbawala, kushirikiana na Brela kuandaa maonesho yatakayowakutanisha wafanyabiashara wa tarafa hiyo na wakala huo.

“Maonesho yawe endelevu, Brela iendelee kwenda kwa wadau wake muhimu na awamu ya pili iwe ya Ubugo hasa wafanyabiashara wa Mbezi na Manzese,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa, amesema maonesho hayo yanayoshirikisha taasisi za Serikali na wajasiriamali mbalimbali yanalenga kutoa huduma za usaidizi kwa wadau waliopata changamoto katika shughuli za biashara.

“Maonesho haya yatafungua njia na Brela itaandaa maonesho mengine ili kuwa karibu zaidi na wadau wake,” amesema Nyaisa.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Woiso inayoshiriki maonesho hayo, Teya Herman, ameipongeza Brela kwa ubunifu wa kuandaa maonesho hayo kwani yatasaidia kuwakutanisha pamoja na wadau mbalimbali wa biashara.

Maonesho hayo yatakayohitimishwa Oktoba 27 kwa kongamano la wadau wa Brela, yanashirikisha taasisi 11 na wajasiriamali zaidi ya 100.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Woiso, Teya Herman, akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, kuhusu bidhaa wanazozalisha wakati wa Maonesho ya Huduma za Brela na Wadau Wake yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City.










Powered by Blogger.