WATANZANIA TUMIENI BANDARI RASMI - TASAC

Ofisa Masoko Mwandamizi wa Tasac, Martha Kelvin, akimweleza Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, shughuli wanazofanya baada ya kutembelea banda la shirika hilo katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA Bombambili, mkoani Geita.

Na Nora Damian, Geita

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limewataka Watazania kutumia bandari rasmi pindi wanapotaka kusafiri ili kuepuka ajali za majini.

Shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2018 linatekeleza jukumu la kuratibu utafutaji na uokoaji baharini, maziwa makuu na maeneo mengine ya maji Tanzania kupitia Kituo cha Utafutaji na Uokoaji Dar es Salaam na Mwanza.

Akizungumza leo Septemba 29,2023 na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini, Ofisa Udhibiti wa Huduma za Bandari Tasac, Victoria Miyonga, amesema kabla chombo hakijasafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni lazima wajiridhishe kwa kupata taarifa kamili ya chombo husika.

“Tunawashauri wananchi wahakikishe wanatumia bandari rasmi kabla ya kuanza safari zao, huwa tuna utaratibu maalumu kabla chombo hakijaondoka tunapata taarifa za kila chombo kinachosafiri.

“Kujua idadi ya abiria, kiasi cha mzigo unaosafirishwa na kuna wenzetu wengine tunaofanya nao kazi wanahakikisha chombo kinachotumika kimesajiliwa na kinatambulika rasmi na wanaokiendesha wana utaalam wa kutosha,” amesema Miyonga.

Ofisa Udhibiti wa Huduma za Bandari Tasac, Victoria Miyonga, akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA Bombambili, mkoani Geita.
 
Ofisa huyo amesema wanashughulika na mnyororo mzima wa usafirishaji kuanzia anayesafirisha, anayehakiki mzigo kwenye shehena, mwenye meli, bandari husika inayopokea mzigo na unakokwenda kuhifadhiwa.

“Tuna jukumu la kulinda masilahi ya watoa huduma kuhakikisha huduma wanazotoa zinakidhi vigezo na masharti ambayo yamewekwa na shirika,” amesema.

Amesema wanadhibiti huduma za bandari na usafiri wa njia ya maji ambapo kuna mawakala wa forodha, meli, wakusanyaji na watawanyaji wa mizigo, wahakiki shehena.

“Tunadhibiti wale wanaopima mizigo inayosafirishwa nje ya nchi, wanaofanya huduma ndogondogo bandarini, tunawadhibiti waendesha bandari kavu. Huwa tunatoa leseni kwa watoa huduma na kuhuhisha au kufuta,” amesema.


Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Tasac, Amina Miruko, amesema wanasimamia na kudhibiti usafiri wa majini kwa kuhakikisha usalama wa vyombo, abiria, mizigo na mazingira yote ya usafirishaji.

“Tunafanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha wanaoviendesha wanakuwa na utaalamu wa kutosha, tunahakikisha kunakuwa na vyombo vya usalama ili inapotokea tatizo au dharura yoyote abiria waokolewe na kutoka salama,” amesema Miruko.

Ofisa Masoko Mwandamizi wa Tasac, Martha Kelvin, amesema wameshiriki maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu wanayotekeleza.

“Tunatoa elimu kwa wananchi na wachimbaji wa Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani kuhusu usafirishaji wa mashine na vifaa vinavyotumika katika kuchimba madini,” amesema Kelvin.







Powered by Blogger.