WENYE CHANGAMOTO YA MIRATHI, ARDHI WAELEZA TAWLA ILIVYOWASAIDIA
Wananchi walionufaika kupitia Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) wameeleza namna walivyonufaika na chama hicho hasa katika masuala ya kisheria.
Takwimu za chama hicho zinaonyesha zaidi ya wananchi milioni 7 wamepatiwa huduma mbalimbali za msaada wa kisheria tangu kilipoanza shughuli zake mwaka 1989.
Leo Mei 22,2025 TAWLA kimefanya kongamano maalumu lililohusisha wadau mbalimbali wakiwemo baadhi ya wananchi walionufaika kupitia huduma zinazotolewa na chama hicho.
Mwema Mwinge ambaye anaishi Temeke, Dar es Salaam amesema alikuwa na changamoto ya mirathi ya marehemu mwanawe na chama hicho kimemsaidia msaada wa kisheria.
"Nilikuwa na changamoto ya mirathi niliyoanza kuishughulikia tangu mwaka 2013 na nilikiwa sina uwezo wa kuweka wakili lakini naishukuru TAWLA imenisaidia mpaka sasa kesi imeisha," amesema Mwinge.
Naye Fatma Dororo mkazi wa Dar es Salaam ambaye alikuwa na changamoto ya mgogoro wa ardhi amesema "Naishukuru TAWLA imenisaidia na mpaka sasa kesi iko mahakama ya rufaa, naomba waendelee kunisaidia kwa sababu sina uwezo wa kumlipa wakili.
Mkurugenzi Mkuu wa TAWLA, Tike Mwambipile, amesema sasa hivi kuna maendeleo makubwa kwa sababu zamani kutokana na mila na desturi watu wengi walikuwa hawatoki kwenda kudai haki lakini sasa hivi wanajitokeza kwa wingi kudai haki.
"Tunataka kuona yeyote ambaye akiona mwenzake anatendewa kitendo cha ukatili wa kijinsia aweze kupata haki zake kwa wakati," amesema Mwambipile.
Amesema pia ili kukabili changamoto ya uhaba wa mawakili wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii iweze kupata ufahamu na kuelewa wanapokutana na changamoto wajue pa kwenda au kujisaidia wenyewe.
"Hata wale wanaokuja kwetu kwa sababu ya uchache wetu si wote tunaweza kuwawakilisha mahakamani kwahiyo, tunawafundisha kwenda kujiwakilisha wenyewe mahakamani. Hii imesaidia sana tumeweza kuwafikia wengi ambao waneweza kwenda kujiwakilisha wenyewe mahakamani," amesema Mwambipile.
Amesema pia wanawatumia wasaidizi wa kisheria ambao wako kwenye jamii ili kutatua changamoto za haraka hatua inayosaidia kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.
