YANGA WAKOSHWA MAAJABU YA TABORA ZOO
Na Beatus Maganja, Tabora
Viongozi na wachezaji wa Timu ya Young Africans (Yanga) wamefanya ziara katika Bustani ya Wanyamapori Hai Tabora maarufu kama Tabora Zoo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza utalii wa ndani na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Ziara hiyo iliyofanywa Aprili 3,2025 iliongozwa na Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, ikijumuisha wachezaji maarufu wa klabu hiyo.
Injinia Hersi Said alisema lengo la ziara hiyo ni kuonyesha mchango wa klabu ya Yanga katika kukuza utalii wa ndani na kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza vivutio vya utalii nchini.
“Ziara yetu hapa ni sehemu ya kuonyesha michango yetu katika kukuza utalii wa ndani, ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vyetu vya utalii, lakini pia kuchangia uchumi wa taifa,” alisema.
Katika kutekeleza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza utalii wa ndani, Rais wa Yanga alitoa wito kwa Watanzania hasa wakazi wa Mkoa wa Tabora na mikoa jirani, kutembelea bustani hiyo ya wanyamapori ili kuendelea kuchangia uchumi wa Taifa akisisitiza kuwa Yanga kama klabu kubwa ya soka nchini, ina nafasi ya pekee kutoa mchango katika masuala ya kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha shughuli za utalii.
Hersi pia aliipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa juhudi zao katika kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya bustani hiyo.
“Pongezi kwa TAWA kwa mapokezi ya kipekee na huduma bora wanazozitoa. Maendeleo haya ni muhimu katika kukuza utalii wa ndani na kufanya vivutio vyetu kuwa vya kimataifa,” alisema.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi na Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo, Wilbright Munuo, alieleza umuhimu wa Bustani ya Wanyamapori Hai Tabora katika kukuza utalii wa ndani.
Munuo alisema bustani hiyo ina mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kutunza rasilimali wanyamapori na kulinda mazingira.
Alitoa wito kwa Watanzania kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa wanyamapori na mazingira yao vinahifadhiwa kwa manufaa ya taifa.
“Tunapaswa kuendelea kutunza wanyamapori wetu ili vizazi vijavyo vione na kufurahia rasilimali hizi. Hii ni sehemu ya kutimiza malengo ya kitaifa ya uhifadhi na maendeleo,” alisema.
Wachezaji wa Yanga pia walionyesha furaha yao kutokana na ziara hiyo na walieleza kufurahishwa na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika bustani ya wanyamapori.
Wachezaji maarufu kama Pacome, Diarra, Jonas Mkude na Clement Mzize walionyesha kuvutiwa na mnyama Simba ambaye ni kivutio kikubwa katika hifadhi hiyo.
Pacome na Diarra walieleza jinsi walivyovutiwa na mandhari ya hifadhi na wanyamapori waliokuwepo, huku wakimtaja mnyama Simba kama mmoja wa wanyama waliowavutia zaidi.
Ziara ya timu ya Yanga katika Bustani ya Wanyamapori Hai Tabora ilifanyika mara baada ya kumaliza mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Tabora United ambapo Yanga ilishinda kwa mabao matatu kwa nunge.


