WATAALAM KUKUTANA KUJADILI MAGONJWA YA MFUMO WA CHAKULA

Na Nora Damian, The Page

Wataalam kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kukutana na kujadili kwa kina namna ya kuendeleza sayansi katika kutibu magonjwa ya mfumo wa chakula (Gastroenterology).

Kongamano hilo litakalofanyika jijini Dar es Salaam Mei 24,2025 limeandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Jamiibora ambayo inajumuisha wataalam wa Kiislamu katika fani za tiba na sayansi shirikishi katika ngazi na taaluma mbalimbali.

Akizungumza leo Aprili 15,2025 Katibu wa Taasisi ya Jamiibora, Dk. Muhidin Mahende, amesema kongamano hilo litawaleta pamoja wataalam wa afya wenye hamasa ya kujifunza na kujadili mwelekeo wa matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa chakula.“Magonjwa ya mfumo wa chakula yanaanzia sehemu ya kinywa mpaka kwenye mfuko wa chakula na tumbo ambako chakula kinameng’enywa, matibabu ya magonjwa kutokana na maendeleo ya teknolojia yanabadilika kila siku hivyo, wataalam watajadili njia tofauti zinazotumika,” amesema Dk. Mahende.

Aidha amesema kutakuwa na mada zitakazowasilishwa moja kwa moja, majopo ya mijadala ya kina, maswali na majibu kuhusu mada zinazohusu masuala ya mfumo wa chakula.

“Tukio hili linatarajiwa kufanyika kwa mfumo wa ana kwa ana na kupitia mtandaoni ili kuruhusu ushiriki wa watu walioko nje ya Dar es Salaam na kutoka sehemu mbalimbali duniani,” amesema Dk. Mahende.


Powered by Blogger.