WASIOFUATA VITAMBULISHO NIDA KUSITISHIWA HUDUMA ZA NAMBA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu zoezi la uchukuaji wa vitambulisho kwa wananchi wanaopata ujumbe mfupi wa simu.


Na Nora Damian, The Page

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema kuanzia Mei Mosi mwaka huu itasitisha matumizi ya namba za utambulisho kwa wale wote ambao walishatumiwa ujumbe mfupi lakini hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao.

Hadi kufikia Machi 23,2025 wananchi 1,880,608 waliokuwa hawajachukua vitambulisho wametumiwa na kupokea ujumbe mfupi wa maneno lakini waliojitokeza kuchukua ni 565,876.

Akizungumza leo Aprili 14,2025 Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema wanalazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kutumia njia mbalimbali kuwafahamisha na kuwahamasisha wananchi kuchukua vitambulisho vyao tangu walipovipeleka katika ofisi za kata, vijiji, mitaa, vitongoji na shehia."Naomba nisisitize kwamba kwa yeyote yule ambaye matumizi ya Namba yake ya Utambulisho wa Taifa yatafungwa, hataweza kuitumia namba hiyo kwa huduma yeyote...ataweza kuitumia tena baada ya kwenda kuchukua kitambulisho chake.

"Ieleweke kwamba kama hujapokea ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) unaokutaka kwenda kuchukua kitambulisho chako, namba yako haitafungwa," amesema Kaji.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuona kila kitambulisho kilichotengenezwa kinachukuliwa na mhusika na hasa ikizingatiwa vimeigharimu Serikali fedha nyingi kuvitengeneza

Mkurugenzi huyo amesema kuanzia Julai mwaka huu wataanza kusajili watu wenye umri chini ya miaka 18 na majaribio yataanza katika Wilaya za Kusini Unguja, Kilolo, Iringa na Rungwe ambapo wanatarajia kusajili watu 235,826 ndani ya miezi miwili.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwezesha upatikanaji wa Jamii Namba pamoja na kundi hilo na kwa wageni wote wanaoingia nchini na kukaa chini ya miezi sita.

Mkurugenzi huyo amesema pia ili kuhakikisha mifumo inasomana tayari NIDA imeunganisha mfumo wake na taasisi 128 za umma na binafsi na wanatarajia hadi kufikia Desemba mwaka huu taasisi hizo zitafikia 200.

Amesema wameweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wadau wanapata huduma yenye kiwango chenye ubora.




Powered by Blogger.