WADAU WAITIKIA WITO WA UONGEZAJI THAMANI MADINI

Kufuatia utekelezaji wa mkakati wa kutosafirisha madini ghafi nje ya nchi, Serikali imewapongeza wadau kwa kuitikia wito wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kujenga viwanda vya uongezaji thamani madini nchini.

Hayo yemesemwa leo na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alipotembelea kujionea ujenzi wa kiwanda cha uongezaji thamani madini ya shaba kilichopo Kata ya Mbugani Wilayani Chunya kinachomilikiwa na Kampuni ya Mineral Access System Tanzania (MAST).

"Mheshimiwa Rais ametuelekeza kuhakikishia tunasimamia sheria na kanuni ili kuwezesha madini kuongezwa thamani hapa nchini kabla yayajasafirishwa nje ili nchi kunufaika na sekta ya madini.

"Tutaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa wadau na wawekezaji wengine walio tayari kuunga mkono jitihada hizi za Mheshimiwa Rais ili kama nchi tupate manufaa zaidi ya kiuchumi ikiwemo kuongeza upatikanaji wa ajira kwa wananchi wetu na kukuza pato la Taifa," amesema Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde alieleza kuwa madini ya shaba yanahitaji kuongezwa kiwango kwa kuchakatwa kufikia asilimia 20 au zaidi ili yaweze kuuzwa nje, na kwamba madini yanayopatikana nchini yana kati ya asilimia 0.5 mpaka 2 na kwamba kiwanda kitakuwa kinazalisha shaba kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 70 na kusisitiza ni mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini.

Vilevile, Waziri Mavunde alioneshwa kufurahishwa na mpango wa Kiwanda cha MAST wa kuhudumia wachimbaji wadogo kupitia kutoa elimu, kugharamia uchimbaji na kuwa soko la shaba yao ya kiwango cha chini ambayo awali walikuwa wakihangaika na soko. Hili litakuwa ni suluhisho tosha kwa wachimbaji wadogo kwani nguvu zao hazitakwenda bure.

Akisisitiza mikakati ya Serikali kwa wachimbaji wadogo, Mavunde alibainisha kuwa Wizara ipo mbioni kuanzisha vituo vya ukodishaji wa mitambo ya uchimbaji nchi nzima ili kusogeza huduma hiyo kwa wachimbaji wadogo na kwa gharama nafuu.
Awali, akimkaribisha Waziri katika kiwanda hicho, Georgefrey Kente ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MAST aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuahidi kwamba kampuni yake inakwenda kujenga viwanda vingine kama hivyo katika Mikoa ya Dodoma na Lindi ili kufikia malengo yao ya uzalishaji.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Chunya ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya, Michombero Anakleth, aliishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa kiwanda hicho kwa kasi kubwa na kueleza bayana kuwa wanaunga mkono kwa asilimia 100 zoezi la ufutaji wa leseni za madini zisizoendelezwa ili wapewe wawekezaji wenye nia njema kwa manufaa ya nchi.


 

Powered by Blogger.