VYUO VIKUU VYAANZA KUCHUANA SAMIA CUP, DIT WALA KICHAPO

Na Nora Damian, The Page

Mashindano ya soka kuwania kombe la Samia ngazi ya elimu ya juu (Elimu ya Juu na Samia Cup) yameanza kutimua vumbi katika viwanja vya Jakaya Kikwete Youth Park ambapo Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imekula kichapo cha mabao 4 – 0 kutoka kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Akizungumza Aprili 14,2025 wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo mgeni rasmi Ofisa Utawala kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Flora Mgonja, amesema Watanzania wanapaswa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi aliyoyafanya hasa katika sekta ya elimu.

“Mheshimiwa Rais ameboresha mazingira kwenye sekta ya elimu, kuna miundombinu ya kutosha, vijana wanafanya vizuri na wengi wanapata mikopo kwahiyo, tuna kila sababu ya kumpongeza,” amesema Mgonja.Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga, amesema wanajivunia juhudi zilizofanywa na Rais Samia kwenye sekta ya elimu ambazo wanatarajia zitawaongezea wapigakura hasa wasomi wa elimu ya juu wakiwemo wa ngazi ya Diploma ambao kwa sasa nao wanapata mikopo. 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Twende Pamoja na Mama Sports Promotions, Mohammed Haji amesema; “Tuliona tuje kwa wanafunzi kwa sababu wanaona kuna mazuri ambayo wanafanyiwa na mama wakaona si vibaya kuja kuyaonyesha kwa vitendo, kwahiyo kama taasisi tutaendelea kumuunga mkono Rais Samia sehemu yoyote ambayo tutaona kuna haja ya kufanya hivyo.

“Zanzibar tumefungua mashindano ya Samia Cup and Mwinyi kwa sababu Dk. Hussein Mwinyi naye kuna mazuri ambayo ameyafanya.Mkurugenzi wa Conel Investment iliyoandaa mashindano hayo, Colnerio Swai, amesema kupitia michezo hasa mpira wa miguu wanaweza kufikisha ujumbe wa mambo yaliyofanywa na Rais Samia kwenye elimu kuanzia msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.

“Kuna mambo makubwa ambayo yamefanyika kwenye elimu ya juu, mikopo imeongezeka, hakukuwa na mikopo ya Diploma lakini mama ameanza kuitoa, kuna miundombinu mingi imejengwa, vifaa vingi vya kufundishia vimenunuliwa watoto wanafanya ‘practical’ za kutosha.

"Imetengenzwa mitaala mizuri inayokwenda na wakati, tukasema tutumie mpira wa miguu kufikisha ujumbe…ajenda yetu ni kusema kwamba asante mama kwa kuleta mazingira mazuri ya elimu kwenye nchi yetu,” amesema Swai.

Kwa mujibu wa Swai, mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka ambapo pia wanatarajia kuhusisha michezo mingine siku zijazo.




Powered by Blogger.