'VIONGOZI WA DINI HAMASISHENI AMANI, MSIJIHUSISHE NA SIASA'
Na Nora Damian, The Page
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Kawambwa amewataka viongozi wa dini kuwahamasisha wananchi wazingatie amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaoatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Alhad Kawambwa ambaye pia ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri neno la Mungu, kuleta amani, umoja na mshikamano wa kitaifa badala ya kujiigiza kwenye siasa na kuleta mgawanyiko kwa waumini.
Ameyasema hayo leo Aprili 23,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la amani kwa viongozi wa dini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 - 2030.
"Viongozi wa dini amani imo mikononi mwenu, ninyi ni wazazi na walezi wa amani, kabla hujasema neno fikiria, zingatia na jiulize nini faida ya neno hilo na ikibidi nyamaza," amesema Sheikh Kawambwa.
Naye Katibu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Askofu Allen Siso, amesema kuelekea katika Uchaguzi Mkuu dhamana ya Tanzania imo kwa viongozi wa dini na kwamba taifa likiharibika wao ndio watakaolaumiwa na likiendelea wao ndio watakaoinuliwa.
Askofu huyo amewataka viongozi wa dini kutambua dhamana waliyonayo na kuwa sehemu ya kutoa majibu ya changamoto za wananchi ili kuhakikisha dunia inabaki kuwa sehemu salama ya kuishi.
"Aliyezaliwa mfalme wa amani mpaka anafufuka (Yesu Kristo) anataka nchi iwe na amani, lakini siku za hivi karibuni tumebadilisha mahubiri yetu kwenye misikiti na kwenye madhabahu tunataka kuingia mahali ambapo hapatupaswi na wala Mungu hajatutuma.
"Tubaki kwenye nafasi zetu na watu watuelewe hivyo kwamba sisi ndio wenye dhamana ya dunia, dhamana ya nchi, kongamano hili liwe la maana kuturudisha kwenye nafasi zetu...tumepewa dhamana ya kuhakikisha dunia inabaki na amani," amesema Askofu Siso.
Akiwasilisha mada katika kongamano hilo kuhusu nafasi ya mwanamke katika kujenga amani, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania, Shamim Khan, amesema ni wajibu wa kila mmoja kuheshimu watawala kwa kuwa kila mamlaka inatoka kwa Mungu.




