UVCCM WAHAMASISHA VIJANA KUJITOKEZA KWA WINGI UBORESHAJI DAFTARI LA MPIGAKURA

Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM, Jesca Mshama, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya umoja huo, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetoa wito kwa vijana wote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika awamu ya pili ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura linaloanza Mei Mosi hadi Julai 4 mwaka huu.

Umoja huo umesema zoezi hilo ni muhimu kwa kila Mtanzania kuhakikisha anapata haki yake ya msingi ya kupiga kura na kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia wa kuamua mustakabali wa nchi kwani haki ya kupiga kura huanza na kujiandikisha.

Akizungumza Aprili 29,2025 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM, Jesca Mshama, amesema kuboresha taarifa ni wajibu wa msingi wa kila kijana mzalendo kwani ni hatua ya kwanza ya kidemokrasia ya kuweza juchaguliwa pia kuchagua viongozi wakati wa uchaguzi."UVCCM tunawakumbusha vijana wote wa Tanzania kwamba kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, asilimia 34.5 ya Watanzania wote ni vijana. Hii inamaanisha vijana ndio nguzo kubwa ya mwelekeo wa Taifa letu. 

"Hivyo tunasisitiza kila kijana mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea, au atakayefikisha miaka hiyo ifikapo siku ya uchaguzi mkuu wa 2025 ajitokeze kuandikishwa," amesema Jesca.

Kulingana na ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mzunguko wa kwanza utahusisha mikoa 15 ya Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe.Mzunguko wa pili utahusisha mikoa 16 ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.

Mzunguko wa tatu utahusisha vituo vya magereza (130 Tanzania Bara) na vyuo vya mafunzo (10 Zanzibar).

Aidha katika awamu hii, jumla ya vituo 7,869 vitatumika Tanzania Bara vituo 7,659 na Zanzibar vituo 210. 

Umoja huo pia umewaonya watu wanaowatumia vijana kufanya vurugu na kuwadanganya wasitimize wajibu wao wa kikatiba au kuwavuruga katika mchakato huo muhimu waache mara moja."Tunawakumbusha kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya sheria na katiba na kila kijana ana haki ya msingi ya kushiriki katika taratibu za kidemokrasia kwa amani, uhuru na utulivu.

"UVCCM tunawaasa vijana wote na wananchi msidanganywe na watu wasio na mapenzi mema na Taifa letu, wanaopotosha dhamira njema ya uboreshaji wa daftari.

"Ni muhimu kila mmoja wetu kujitokeza na kutimiza wajibu huu wa kizalendo na kidemokrasia kwa mustakabali bora wa taifa letu. Tanzania imara, maendeleo endelevu, yanaanza kwa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa kitaifa," amesema.

Pia ametoa wito kwa vijana kuwa wazalendo wa kweli, kulitumikia taifa kwa upendo na kuhakikisha wanalinda na kudumisha amani ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan (Novemba 2020 hadi Februari 2025), ajira zaidi ya milioni 8 zimezalishwa, sawa na utekelezaji wa asilimia 11 ya lengo la kutengeneza ajira milioni 7 katika sekta ya umma na binafsi. Amesema ajira hizo zimezalishwa kupitia miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Reli ya Kisasa ya SGR, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato pamoja na fursa za ajira katika sekta za elimu na afya.

Amesema pia kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri zote nchini vijana wengi wamewezeshwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na kujipatia kipato halali ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2024 zaidi ya Sh bilioni 250 zimetolewa kwa vikundi vya vijana.

"UVCCM tunawataka vijana wote wa Kitanzania kuchangamkia fursa hizi, kuwa wazalendo kwa taifa lao, na kamwe wasikubali kutumika vibaya na watu wasiolitakia mema taifa letu. Ushiriki wetu wa sasa ndio unaojenga Tanzania ya kesho yenye nguvu, haki, maendeleo na amani ya kudumu

"Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha mfano wa uongozi bora unaoweka mbele masilahi ya vijana na Watanzania wote kwa kujenga Tanzania mpya yenye misingi ya maridhiano, utawala bora, heshima ya haki za binadamu na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii," amesema.

Umoja huo pia umetoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge kwa kuwa Tanzania ya sasa inahitaji viongozi vijana wenye maono mapana, weledi, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa taifa.

"Kila kijana ajiandikishe na kuhakikisha taarifa zake ziko sahihi, kila kijana mwenye nia ya uongozi ajitokeze kugombea, tuonyeshe uzalendo wetu kwa kulitumikia taifa kwa uadilifu, uchapakazi na mshikamano," amesema.

Katika hatua nyingine Jesca amesema katika kuendelea kuimarisha uhai wa Jumuiya hiyo na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya vijana nchini, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida, ameendelea na ziara maalumu iliyoanza Aprili 2025.

Ziara hiyo ilianzia katika Mkoa wa Njombe kisha Geita, Mwanza na leo anaendea Mkoa wa Simiyu kisha atakwenda Shinyanga na Tabora.




Powered by Blogger.