UNGENI MKONO KAMPENI YA USAFI - DC MPOGOLO
Wananchi na viongozi wa Serikali za mitaa katika Halmashari ya Jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuendelea kuunga mkono kampeni ya usafi ya kila Jumamosi ili kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi wakati wote.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alipozungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi wa kila Jumamosi katika fukwe za Bahari ya Hindi eneo la Dengu.
Mpogolo amesema ili kampeni hiyo ilete matokeo chanya ni vema kila mmoja akatimiza wajibu wake kuhakikisha maeneo yote yanakuwa safi.
Amesema ufanisi mzuri katika zoezi la usafi utasaidia kujilinda na kujikinga na magonjwa ya mlipuko hasa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea katika maeneo mbalimbali.
Aidha amesisitiza juu ya umuhimu wa kutunza fukwe za bahari pamoja na rasilimali za bahari zinazoweza kutumika kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa kwa kukuza uchumi.
Amesema kufanya usafi katika fukwe za bahari kunasaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangia bahari kuharibika.
Viongozi wengine walioshiriki zoezi hilo la usafi ni pamoja na Mkurugenzi wa Jiji Elihuruma Mabelya, Katibu Tawala Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani, viongozi wa mitaa, wakandarasi na wananchi mbalimbali.
Zoezi hilo la usafi limeanzia makutano ya Barabara ya Kamata kuelekea Utumishi, Terminal 1 kuelekea katikati ya mji na kumalizika katika eneo la Dengu fukwe za Bahari ya Hindi.
