TANESCO YAANZA KULIPA FIDIA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI MIRADI YA UMEME

Mtwara, Ruvuma

📌Ni mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 Tunduru -Masasi

📌Sh bilioni 4.7 kutumika kulipa fidia

📌Wananchi waahidi kuyahama maeneo ndani ya siku 30 walizopewa

Jumla ya wananchi 1,526 wanatarajia kunufaika na malipo ya fidia ya Sh bilioni 4.7 baada ya kupisha mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wenye msongo wa kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi na ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha Masasi kilichopo mkoani Mtwara.

Akizungumza baada ya wananchi kukabidhiwa hundi April 26,2025 Mwenyekiti wa Kijiji cha Sululu, Venant Kamtahule, amesema ujenzi wa miradi hiyo ilumelenga kuimarisha upatikanaji wa umeme utakaochochea shughuli za kiuchumi na uwekezaji wa viwanda vya kubangua korosho.

"Tunaishukuru sana TANESCO wananchi wangu takribani 16 wa Kijiji cha Sululu wamenufaika na malipo ya fidia, haya ni mafanikio makubwa tuliyokuwa tukiyasubiri kwa muda mrefu. Tunaimani mradi huu utaongeza chachu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi,’’ alisema Venant. Naye Meneja wa TANESCO wilayani Masasi, Mhandisi Kidala Maeda, amesema zoezi hilo la ulipwaji fidia lilianza April 25,2025 na hatua hiyo itamwezesha mkandarasi kuendelea na ujenzi hususani katika kituo cha kupoza umeme cha Masasi ambao utekelezaji wake uko katika hatua za awali.

"Mikoa ya Lindi na Mtwara bado haijaunganishwa na Gridi ya Taifa tunatumia mashine za gesi kutoka Mtwara, lakini Serikali imeona ni wakati sasa na sisi watu wa Kusini tupate umeme kupitia Gridi ya Taifa ili tunufaike na umeme unaozalishwa kutoka katika mradi wa kufua umeme wa bwawa la Julius Nyerere ambao umekamilika,’’ alisema Kidala.Mradi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Masasi utagharimu zaidi ya Sh bilioni 70 ambapo vijiji 43 vinapitiwa na mradi huo katika Wilaya za Masasi, Nanyumbu na Tunduru.

Powered by Blogger.