ROBO FAINALI ELIMU YA JUU SAMIA CUP KANYAGA TWENDE

Na Nora Damian, The Page

Kivumbi cha mashindano ya soka yanayoshirika vyuo vikuu vya jijini Dar es Salaam (Elimu ya Juu Samia Cup) kimeendelea kushika kasi kwa timu zilizotinga hatua ya robo fainali.

Robo fainali hizo zimeanza kuchezwa leo Aprili 27,2025 katika viwanja vya Jakaya Kikwete na kushuhudia Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kikishindwa kutamba mbele ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kutandikwa mabao 3 - 2.

Katika mchezo mwingine Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) kimeishindilia Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) mabao 5 - 4 ambayo yamepatikana kwa mikwaju ya penati.Kutokana na ushindi huo UDSM na KIU zimetinga nusu fainali ya mashindano hayo.

Kocha wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Michael Francis amesema; "Tumeanza mashindano tukiwa na malengo makubwa lakini hii ni michezo hivyo, ni lazima kuheshimu matokeo. Tulianza vizuri kwenye kundi na kuongoza vizuri, hatukupoteza mpaka leo tumekuja robo fainali tukiamini kwamba tutafanya vizuri.

"Wachezaji walikuwa timamu lakini wakati mwingine sintofahamu za mchezo unaweza kutoka mchezoni ndiyo matokeo ya mchezo. Kwahiyo tunashukuru kwa kushiriki," amesema Francis.Meneja wa Conel Investment waandaaji wa mashindano hayo, Mirumbe Chacha, amesema mashindano hayo yamejikita zaidi kwa vyuo vikuu vilivyopo jijini Dar es Salaam ambapo yanahusisha vyuo 16.

"Mashindano ni mazuri na yana mwamko mkubwa kwa sababu watu wengi wameyapokea katika mtazamo chanya, tunawakaribisha wanafunzi wa vyuo vyote vinavyoshiriki, wadau, Serikali na wana jamii kwa ujumla katika hatua zilizosalia ili kuunga mkono juhudi za mheshimiwa Rais Samia kwa kuboresha mazingira ya elimu nchini," amesema Chacha.


Powered by Blogger.