RC CHALAMILA AWATOA HOFU WAFANYABIASHARA, WAWEKEZAJI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya mkoa huo. 


Na Nora Damian, The Page 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewatoa hofu wafanyabiashara na wawekezaji kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu akisema jiji hilo litaendelea kuwa na amani wakati wote hivyo wawe huru kufanya shughuli zao.

RC Chalamila ameyasema hayo leo Aprili 18,2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya mkoa huo. 

Amesema chama chochote cha siasa, taasisi ya dini, isiyo ya dini, mtu binafsi, shirika au kampuni hakuna atakayeweza kuvuruga amani ambayo imekwisha jengwa katika misingi ya uongozi na hasa uongozi bora wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.“Tunafahamu wapo baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa na malalamiko yao wazingatie sheria, utaratibu wa namna ya kufikisha kwenye vyombo na taasisi zinazohusika ili kuwa na uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia unaokidhi vigezo vya utawala bora,” amesema Chalamila. 

Kuhusu Soko la Kariakoo, amesema kinachoendelea kwa sasa ni ukamilishwaji wa ujenzi wa uzio ili kutoruhusu kuvamiwa na kuchafuliwa kwa biashara zisizo rasmi na kuwaomba viongozi wa wafanyabiashara wadogo wadogo Kariakoo kufungua njia ili soko hilo liweze kupitika kirahisi.

Amesema pia tayari wafanyabiashara waliokuwepo zamani zaidi ya 1,500 wamehakikiwa na kuendelea kuonyeshwa vizimba na utaratibu utakaotumika kuingia sokoni hapo.

Aidha amesema jiji hilo kwa sasa linaendelea na utekelezaji wa miradi ya madaraja, barabara za lami, kuimarisha vivuko, kuhamisha baadhi ya miundombinu katika barabara kama vile ya Dawasa na umeme ili kupisha ujenzi wa miradi inayoendelea. 

Kuhusu ujenzi wa Daraja la Jangwani amesema mkandarasi amekwishaanza kujenga kambi ya ujenzi na wakati wowote daraja hilo litaanza kujengwa na kuwataka wananchi kuongeza kasi ya kulipa kodi ili kupata maendeleo yaliyokusudiwa. 

Mkuu huyo wa mkoa amesema pia hivi karibuni watafanya operesheni ya kuwaondoa ombaomba kwa kuwa wamebaini wanatumika kibiashara huku wengine wakiwa wanaishi katika nyumba za kulala wageni.


Powered by Blogger.