MAMA ONGEA NA MWANAO WATIA MGUU TAMASHA MTOKO WA PASAKA, WAHIMIZA AMANI
Na Nora Damian, The Page
Maandalizi ya Tamasha la Mtoko wa Pasaka yamezidi kushika kasi baada ya Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kutangaza kushiriki.
Tamasha hilo lililoandaliwa na Mwanamuziki wa Injili, Christina Shusho linatarajiwa kufanyika Sikukuu ya Pasaka jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano na waandishi wa habari leo Aprili 8,2025 Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, amempongeza Shusho kwa kuandaa tamasha hilo na kuwahamasisha watu mbalimbali kushiriki.
"Tunahitaji kumpongeza Shusho kwa juhudi alizozifanya kwa kuunganisha wanamuziki mbalimbali...hachuji," amesema Steve.
Aidha amesema kaulimbiu ya tamasha hilo 'Kwa maombi tutashinda' ni muhimu kwa kuwa maombi yana nguvu na kwamba amani na utulivu unatakiwa kulindwa kwa gharama yoyote, si kwa mtutu bali kwa kuomba.
Steve amesema kama taasisi wanahakikisha wanaongea na Watanzania kwa vitendo kupitia miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo wanatarajia kutoa vifaa vya kujifungua katika hospitali zote za wilaya jijini Dar es Salaam kuwasaidia wajawazito wasiokuwa na uwezo.
Naye Shusho amesema tamasha hilo litahusisha wanamuziki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na kuwahamasisha Watanzania kujitokeza kushiriki kwa wingi.
