WATAALAM WA KOROSHO WAJENGEWA UWEZO KUONGEZA UFANISI
Katika jitihada za kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa zao la korosho wataalam 75 kutoka katika nchi tisa za Afrika wanajengewa uwezo ili kufikia malengo ya kukuza zao hilo.
Kati ya nchi hizo sita ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaani Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania, Burundi na Sudani Kusini.
Akizungumza Machi 24,2025 Mwakilishi wa Bodi ya Korosho (TCB), Dk. Rashidi Tamatama, amesema mafunzo hayo ya wiki moja yataimarisha uzalishaji na masoko ya zao hilo.
"Mwaka 2024/2025 tumezalisha tani 528,000 baada ya Serikali kutoa ruzuku ya viuatilifu na malengo ya msimu wa 2025/2026 ni kuzalisha tani 700,000 na tani milioni moja ifikapo 2030," amesema Dk. Tamtam.
Hata hivyo amesema licha ya kuongezeka kwa uzalishaji mikakati waliyonayo sasa ni kuuza korosho ambayo tayari imebanguliwa badala ya kupeleka korosho ghafi.
Kwa mujibu wa Dk. Tamtam, katika korosho zilizozalishwa msimu wa 2024/2025 ni asilimia 10 tu ndiyo iliyobanguliwa na kutokana na mikakati iliyopo wanatarajia kufikia 2030 wawe wanabangua korosho yote inayolimwa nchini.
"Tunashukuru kufanyika kwa mafunzo haya Tanzania kwa sababu itasaidia katika kupanga mikakati itakayotuwezesha kufikia malengo ambayo tumejiwekea," amesema.
Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Fahari Marwa, amesema wanafarijika kuwa sehemu ya mpango huo ambao ulianza tangu 2014 na hadi sasa una wataalam zaidi ya 1,300 ambao wamenufaika.
Amesema wanaamini wataalam watakaonufaika kupitia mafunzo hayo watakuwa chachu ya kuendeleza mpango mkakati wa zao la korosho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Julwaa la Korosho Afrika (ACA), Ernest Mintah, amesema licha ya ongezeko la uzalishaji wa korosho katika Bara la Afrika bado kuna changamoto ya usindikaji wa korosho ghafi hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha uzalishaji na kuzitafutia suluhu changamoto nyingine.
Profesa Edda Lwoga ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, amesema mafunzo hayo yataboresha kilimo na sekta nzima ya korosho.
"Tunategemea baada ya mafunzo wataweza kuangalia changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kwenye nchi wanakotoka na kuja na suluhisho la kujua masoko mazuri yako wapi, bei na vitu vingine," amesema Profesa Lwoga ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
