NAMBA MPYA HUDUMA KWA WATEJA TANESCO IRAHISISHE UTATUZI WA CHANGAMOTO - KAPINGA
Na Nora Damian, The Page
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka mameneja wa mikoa na wilaya wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuhakikisha changamoto za wateja zinatatuliwa kwa usahihi na kupunguza malalamiko ya kutofikiwa kwa wakati.
Ameyasema hayo leo Machi 12,2025 wakati wa uzinduzi wa namba mpya ya huduma kwa wateja (180) itakayotumiwa na wateja bila malipo ili kupata huduma mbalimbali kupitia kituo cha miito ya simu cha TANESCO.
Amesema Serikali imedhamiria Watanzania wapate huduma bora ya umeme na kuhakikisha wanatatuliwa changamoto zao kwa kupiga simu hiyo bila malipo.
"Wateja wahudumiwe na kupewa majibu mazuri na kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa. Mameneja wa mikoa na maafisa huduma kwa wateja wasimamie kwa karibu watoa huduma ili kuendelea kulipa taswira nzuri shirika letu.
"Nasisitiza kuimarishwa kwa utoaji wa huduma ambao unakidhi mahitaji, lugha na namna ya kuwahudumia wateja wetu tuendelee kuzingatia kwa ufanisi. Hatutavumilia huduma ambayo haikidhi vigezo kwa wateja wetu..wateja wanapotoa taarifa za changamoto zao zitatuliwe kwa usahihi ndani ya masaa manne ambayo tulikubaliana," amesema Kapinga.
Aidha amesema mpango wa Serikali wa kuhakikisha vijiji vyote nchini vinafikiwa na umeme umekamilika na kazi iliyobaki ni kusambaza kwenye vitongoji ili kuwezesha Watanzania wote kupata umeme na kuutumia kwa shughuli mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa TANESCO, Gissima Nyamo - Hanga, amesema kuzinduliwa kwa namba hiyo mpya ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya wizara kuhakikisha mteja anapopiga simu hatozwi gharama zozote na namba hiyo itakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wateja wengi kwa wakati mmoja.




