MAJI KUWAFIKIA WANANCHI KWA ASILIMIA 100
Serikali inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za maji safi na salama ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa asilimia 100.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi ya Ziwa Victoria kutoka eneo la Makomero - Mgongoro, Kijiji cha Mwamayoka, Igunga mkoani Tabora mradi wenye thamani ya Sh milioni 840.8 utakaonufaisha zaidi ya wakazi 5,000.
“Mradi huu ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuweni na uhakika kwamba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni kutekeleza majukumu yenu ipasavyo kwa sababu tunaye kiongozi madhubiti," amesema Majaliwa.
Ameuagiza Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) kusogeza vituo vya umma vya kuchota maji karibu na wananchi.
Ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 80 na unahusisha ujenzi wa vituo sita vya umma vya kuchota maji, ukarabati wa vituo sita vya umma kuchota maji, ukarabati wa mabirika mawili ya maji kwa ajili ya mifugo, kuchimba mitaro ya kulaza bomba na kufukia mitaro mita 25,000.
Naye Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema wizara hiyo itaendelea kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji inaendelea kuimarika ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanatenda haki na kuepuka kuwabambikizia wananchi ankara za maji.