INSPEKTA KATO AELEZA DAWATI LA JINSIA NA WATOTO LINAVYOKABILI UKATILI WA KIJINSIA

Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Inspekta wa Polisi, Mdathiru Kato, akizungumza kuhusu majukumu ya dawati hilo na umuhimu wa kuripoti ukatili wa kijinsia.


Na Nora Damian, The Page

Wananchi wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia wametakiwa kupaza sauti zao hasa katika Dawati la Jinsia na Watoto ili changamoto zao ziweze kutatuliwa.

Wito huo umetolewa na Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Inspekta wa Polisi, Mdathiru Kato, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya dawati na umuhimu wa kuripoti ukatili wa kijinsia.

Amesema matukio yanayoripotiwa kwa wingi katika dawati hilo ni yale yanayotokana na ukatili wa kimwili kama vile vipigo na ukatili wa kingono yaani ubakaji na ulawiti.

"Jamii iko kwenye mmomonyoko mkubwa wa maadili, matukio ya ubakaji, ulawiti yamekithiri kwenye jamii. Tunakwenda kutoa elimu unakuta watoto wadogo shule za msingi wameathiriwa wameshalawitiwa, watoto wa kike wamebakwa."Jamii ifunguke ifike kwenye madawati ya jinsia na watoto, kila unapoona kituo kikubwa ujue kuna dawati la jinsia na watoto. Ni kitengo maalumu ambacho kina wataalam na wahudumu waliopewa mafunzo maalumu," amesema Inspekta Kato.

Aidha amesema kanda hiyo ina madawati 28 ambapo wamekuwa wakizingazia usiri na faragha katika kuhudumia wateja na kwamba wanasikiliza mashauri yote yanayohusu familia, watoto, wanawake, wanaume.

Kwa sasa kuna madawati ya jinsia na watoto zaidi ya 400 nchi nzima ambayo yamesaidia kutoa hamasa kwa jamii na wananchi kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia.


Powered by Blogger.