ETDCO WAKAMILISHA MRADI WA KILOVOLTI 132 TABORA - URAMBO

Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme ( ETDCO) imefanikiwa kuwasha rasmi laini ya msongo wa Kilovolti 132 yenye urefu wa kilomita 115 kutoka Tabora hadi Urambo.

Laini hiyo inakwenda kuwasaidia wananchi wa Urambo na Kaliua kupata umeme wa uhakika na kuchochea maendeleo.

Akizungumza leo Machi 20, 2025 mkoani Tabora katika zoezi la kuwasha laini hiyo mpya ya Tabora hadi Urambo, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya ETDCO, CPA Sadock Mugendi, ameishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kuwaamini kutekeleza mradi huo, huku akieleza kuwa wananchi wa Wilaya ya Urambo na Kaliua wategemee kupata umeme wa uhakika.CPA Mugendi amesema kuwa mradi huo umetekelezwa na watalaamu wazawa jambo ambalo limeonesha wanaweze kutekeleza miradi ya umeme kwa wakati bila tatizo lolote.

Meneja wa Mradi wa Tabora- Katavi kwa upande wa TANESCO, Mhandisi Sospeter Oralo, amesema umegharimu Sh billioni 40, ambapo gharama ya laini yenye msongo wa Kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Urambo ni Sh bilioni 24, huku ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Urambo zimetumika Sh bilioni 16 fedha ambazo zimetoka Serikali ya Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi Huduma za Ufundi ETDCO, Mhadisi Dismas Massawe, amesema baada ya kuwasha laini hiyo wananchi wa Urambo na Kaliua watarajie kupata umeme wa uhakika kupitia kituo cha Uhuru Wilaya urambo chenye mashine umba (transformer) ya megawati 28.

Naye Meneja wa Mradi wa Tabora hadi Urambo upande wa ETDCO, Mhandisi Ntuli Burton, amesema mradi huo ulianza Aprili 2024 na walitegemea kumalizika June 2025. "Tunashukuru Mungu tumefanikiwa kumaliza mradi kabla ya wakati ili wananchi wa Urambo waweze kupata umeme wa uhakika haraka iwezekanavyo," amesema.

Mradi huo wa kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Urambo wenye msongo wa kilovolti 132 utasiadia kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Urambo, Kaliua pamoja na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.


Powered by Blogger.