ALAT YAWATAKA MADIWANI KUELEZA MEMA YALIYOFANYWA NA RAIS SAMIA
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) imewataka madiwani nchini kufanya mikutano ya hadhara kwenye vijiji, mitaa na vitongoji ili kuwaeleza wananchi mema yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na jinsi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ilivyotekelezwa kwenye maeneo yao.
Hivi karibuni wakati wa mkutano wa 39 wa ALAT uliofanyika jijini Dodoma Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maagizo kadhaa kwa jumuiya hiyo likiwemo la kueleza kwa umma utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye maeneo yao.
Akizungumza leo Machi 19,2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Murshid Nzege, amesema fedha nyingi zimepelekwa kwenye mamlaka mbalimbali nchini kutekeleza miradi ya maendeleo na kazi kubwa imefanyika.
“Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan ameleta fedha nyingi za maendeleo kwenye mamlaka zetu, tumetekeleza miradi mikubwa, nitoe wito kwa waheshimiwa madiwani kuanza kufanya mikutano ya hadhara kwenye vitongoji, vijiji, mitaa na makundi mbalimbali ili kuwaeleza mema yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita na jinsi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ilivyotekelezwa kwenye maeneo yetu.
“Yapo yanayoonekana kwa mfano majengo, vyoo, barabara za lami zinaonekana lakini yapo ambayo hayaonekani mfano ajira. Wakati anaingia madarakani mwaka 2021 tulikuwa na uhaba mkubwa wa watendaji wa vijiji na mitaa lakini leo hakuna,” amesema.
Ametoa mfano wa Halmashauri ya Bukoba anakotoka yeye kwamba ina vijiji 94 lakini kulikuwa na upungufu wa watendaji wa vijiji 40 lakini leo hakuna kijiji ambacho hakina mtendaji.
“Tulikuwa na upungufu mkubwa wa walimu, wahudumu wa afya wameajiriwa, kipato kwa wananchi kimeongezeka, kwenye kilimo mfano kahawa wakati anaingia madarakani kilo moja ilikuwa inauzwa Sh 2100 hadi 2500 lakini sasa hivi inauzwa kati ya Sh 5,500 hadi 6,000 kwahiyo kipato cha mtu mmoja mmoja kimeboreshwa,” amesema.
Maagizo mengine ni kuongeza umakini katika ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi, kuweka mipango ya halmashauri kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kubuni vyanzo vipya vya mapato ili halmashauri zianze kujitegemea na kuacha kutegemea, usimamizi wa sheria hasa idara ya ardhi katika kutoa vibali vya ujenzi, sheria ya uwekezaji, kutenga maeneo ya uwekezaji.
Jumuiya hiyo pia inatarajia kujenga jengo la kitega uchumi la ALAT lenye zaidi ya ghorofa nne na kwamba tayari wana eneo lenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 6,000 jijini Dodoma.
