TAFSIRI YA TUZO ALIYOPEWA RAIS SAMIA THE GATES GOALKEEPER
Na Nora Damian, The Page
Mwaka 2016 nilisafiri kwenda katika Kijiji cha Ikuza kilichopo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambacho kipo kisiwani na wakati huo hakikuwa na zahanati hali iliyosababisha wananchi hususan kina mama wajawazito na watoto kushindwa kupata huduma za afya ipasavyo.
Ili kuweza kukifikia kijiji hicho nilisafiri kwa kutumia boti kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita hadi Kijiji cha Ikuza mwendo wa dakika 52 safari ambayo haikuwa rahisi sana kutokana na changamoto za hali ya hewa siku hiyo zilizosababisha kuwepo kwa mawimbi makubwa Ziwa Victoria.
Hali hii ndiyo ambayo walikuwa wakikumbana nayo wananchi wa Kijiji cha Ikuza na kulazimika kusafiri kwa saa tatu kufuata huduma za afya katika kituo kinachomilikiwa na Kanisa la AICT kilichopo Kasenyi huku usafiri pekee ukiwa ni boti.
Changamoto hiyo ilisababisha baadhi ya wanawake kujifungulia njiani wakiwa kwenye boti kwa sababu wakati mwingine walilazimika kusubiri kwa saa kadhaa boti ijaze abiria hali ambayo ilichangia kushindwa kufika hospitali kwa wakati.
Kwa sasa Kijiji cha Ikuza kina zahanati ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hasa kina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Kero waliyokuwa wakiipata wananchi wa Ikuza ni mfano wa hali ilivyokuwa katika maeneo mengi ya nchi wakati huo ambapo Tanzania ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama na watoto chini ya miaka mitano.
Takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonyesha vifo vya akina mama vilikuwa 556 kwa kila vizazi hai 100,000 wakati kwa watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 67 mwaka 2015/2016 kwa kila vizazi hai 100,000.
Miaka sita baadaye (mwaka 2022) takwimu hizo zimebadilika kwa vifo kupungua na kufikia 104 kwa kila vizazi hai 100,000 huku vya watoto vikikupungua hadi kufikia 43.
Hii ni kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali hasa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ikiwemo kujenga miundombinu, kununua vifaa tiba, kusomesha wataalam na kuajiri wahudumu wa afya wa ngazi zote.
Jitihada hizo ndizo ambazo zimemwezesha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutunukiwa Tuzo Maalumu ya Kimataifa ya The Gates Goalkeeper Award na Taasisi ya Gates ya Marekani.
Rais Dk. Samia ambaye ni kiongozi wa kwanza barani Afrika kupokea tuzo hiyo, ametunukiwa katika kipengele cha mapambano dhidi ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga chini ya miaka mitano.
Taasisi ya Gates wameangalia zaidi jitihada anazozifanya Rais Dk. Samia katika mapambano ya afya ya uzazi ambayo yamewezesha kubadili namba za Tanzania katika historia ya dunia kwa habari ya vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano.
Itakumbukwa pia mwaka 2018 akiwa Makamu wa Rais, Dk. Samia alizindua kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ iliyolenga kuhimiza uwajibikaji wa viongozi na watendaji ndani ya sekta ya afya kushughulikia changamoto za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kuweza kufikia Malengo Endelevu ya 2030.
Shabaha ya Malengo Endelevu ya Dunia ya Mwaka 2030 ni kupunguza vya kinamama wakati wa kujifungua hadi kufikia 70 kwa kila vizazi hai 100,000 na kwa takwimu za sasa za Tanzania maana yake inapambana na vifo 34 kuweza kulifikia lengo hilo au kuvuka kwa kutokuwa na kifo kabisa.
Rais Dk. Samia anasema simulizi ya Tanzania ni ushuhuda wa kinachowezekana iwapo afya, lishe na usawa vitapewa kipaumbele.
Anasema Serikali imeweka mipango madhubuti ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 Tanzania inavuka lengo la kimataifa la kupunguza vifo vya akina mama, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.
“Tuzo hii ina maana kubwa, dunia imetambua jitihada zetu katika kuboresha huduma za afya hasa ya mama na mtoto. Miaka minne iliyopita vifo vya akinamama wakati wa kujifungua vilifikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Kwa sababu ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, kujenga miundombinu, kununua vifaa tiba, kusomesha wataalam na kuajiri wahudumu wa afya wa ngazi zote tumeweza kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
“Kwa akina mama tumevishusha kutoka 556 hadi 104, lengo la kimataifa la mwaka 2030 ni kufikia vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000…kwa mwenendo huu tutafikia au hata kuvuka lengo hilo,” anasema Rais Dk. Samia.
Anasema kwa watoto chini ya miaka mitano vifo vimepungua kwa kiasi kikubwa lakini bado wanakabiliana na changamoto kwa watoto wachanga ambao wengi hupoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya dawa za kienyeji na kuchelewa kufika hospitali.
Rais Dk. Samia anasema pia awali hakukuwa na vifaa vya kutosha kuokoa maisha yao lakini kwa sasa wamewekeza kwenye ununuzi wa vifaa na kuahidi kuwa haali itazidi kuimarika.
Anasema ingawa uongozi wake umechangia mafanikio hayo lakini tuzo hiyo ni heshima kwa Watanzania wote hasa watumishi wa sekta ya afya katika ngazi zote ambao wamewezesha huduma za afya bora kuwafikia wananchi.
“Nataka kuitoa tuzo hii kwa wafanyakazi wote wa sekta ya afya ambao utu wao, ujuzi na ustahimilivu umefanya jitihada zetu ziwe na maana. Tutaendelea kupaza sauti juu ya maendeleo ya kimataifa na kuhakikisha kwamba afya bora inabaki kuwa haki kwa wote.
“Tunatoa wito wa kuendelea kushirikiana, ni lengo langu kufanikisha uwekezaji endelevu, kama jumuiya ya kimataifa sote tuna wajibu wa kuhakikisha hakuna mwanamke mtoto au kijana anaachwa nyuma,” anasema Rais Dk. Samia.
Rais Dk. Samia anaendelea kuweka rekodi ya kuokoa uhai wa Watanzania kwa hakikisho la huduma bora za afya hasa za uzazi kwa kuwa hakuna mwanamke anayepaswa kufa wakati wa kujifungua.
