PIC YARIDHISHWA UTEKELEZAJI MIRADI YA TAWA MAKUYUNI
Na Beatus Maganja - Arusha
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustine Vuma amesema wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya utalii inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika Hifadhi ya eneo la Makuyuni iliyopo Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
Vuma ameyasema hayo Februari 9,2025 wakati kamati hiyo ilipotembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na TAWA katika eneo hilo.
"Kamati imefurahishwa na namna ambavyo miradi inaendelea, ikumbukwe kwamba eneo hili mara ya kwanza lilikuwa chini ya mwekezaji kwa muda mrefu, baada ya Serikali kuona hakuna tija eneo liliendelea kukaa kwa mwekezaji, ikalichukua na kukabidhiwa msajili wa hazina lakini baadaye aliwakabidhi TAWA ili waweze kuliendeleza.
"Kamati imeona na imeshuhudia pasipo na shaka kwamba uwekezaji unafanyika kwa utaratibu ambao unafaa, tija ya uwekezaji ipo kwa sababu mapato yameanza kuongezeka na tunaamini yataendelea kuongezeka. Kwahiyo TAWA wataendelea kufanya uwekezaji kwa sababu tumeona imeanza kulipa," amesema.
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa Watanzania na wakazi wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani kutembelea eneo hilo ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.
"Makuyuni Wildlife Park ni sehemu nzuri ya kuja kutembelea, ukija hutamani kutoka, kuna wanyamapori wa kila aina, kuna twiga, tumeona simba, tembo, swala kwakweli ni kituo cha kuvutia watalii," amesema.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, amesema tangu TAWA ikabidhiwe eneo hilo idadi ya wanyamapori imeongezeka na fedha zinazotokana na uwekezaji uliofanyika zimeongezeka.
Amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja TAWA imekusanya zaidi ya Sh milioni 200 jambo linalithibitisha kuwa ni mwanzo mzuri na wenye kuleta matumaini makubwa.
Amesema kutokana na uwekezaji unaondelea kufanywa na TAWA wizara inatarajia kuongeza mapato ya zaidi ya billioni 20 kwa mwaka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Meja Jenerali mstaafu, Hamis Semfuko, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia TAWA eneo la Makuyuni ili iweze kulitumia kwa shughuli za utalii.
Amesema TAWA imejijengea utamaduni wa kuwa na matumizi sahihi ya fedha hasa zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
"Hii ndio tabia yetu TAWA kuhakikisha kwamba kila senti ambayo mheshimiwa Rais anaitoa inatumika kama ilivyopangwa na kwa ubunifu mkubwa," amesema Semfuko.



