OPARESHENI KUDHIBITI FISI YAVUNA 16 SIMIYU

Na Mwandishi Wetu, Simiyu

Oparesheni maalumu ya kuwadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu aina ya fisi waliokuwa wanaleta taharuki na madhara kwa jamii inayoendelea mkoani Simiyu imeonesha mafanikio makubwa baada ya fisi 16 kuvunwa.

Hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inalenga kuhakikisha usalama na utulivu kwa wananchi vinarejea.

Hayo yamesemwa Februari 19, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, alipokuwa akiongea na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.

Kihongosi amesema kufuatia changamoto hiyo, Serikali ilichukua jukumu kubwa la kuhakikisha inalinda wananchi wake ikiwemo kuanzisha oparesheni maalumu inayohusisha Jeshi la Uhifadhi Kwa Taasisi za TAWA, TANAPA na TFS kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi, oparesheni inayotajwa kuanza Januari 25, 2025."Tarehe 20 mwezi wa kumi na mbili mwaka jana baada ya fisi kuvamia wananchi Serikali ilichukua hatua kubwa ya kushirikisha vyombo vyake (TAWA na Jeshi la Polisi) na kuanza oparesheni, lakini ilipofika tarehe 25 mwezi wa kwanza mwaka huu, oparesheni ya mkoa mzima ilifanyika kwa ukubwa kuhakikisha inakabiliana na fisi wote waliokuwa wanasumbua wananchi.

"Tangu kuanza kwa oparesheni hii vyombo vyetu vimeweza kudhibiti na kuua fisi 16 na ndio maana kwa sasa hali imetulia," amesema Kihongosi.

Amewatoa hofu wananchi wa mkoa huo akisisitiza kuwa hali ni shwari na kuwataka waendelee na shughuli zao kama kawaida huku akikemea vikali imani za kishirikina kuhusiana na mnyamapori fisi kwa baadhi ya wakazi wa Simiyu na kuwataka wote wanaofuga wanyamapori pori hao kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria kumiliki nyara za Serikali bila kibali.Kwa upande wake Ofisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja, amewaomba wananchi wa Mkoa wa Simiyu hususani Wilaya ya Itilima kuacha tabia ya kutembea nyakati za usiku na alfajiri kwani ni nyakati ambazo fisi huwa katika mawindo yao.

Vilevile amewasisitiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa maofisa wa Jeshi la Uhifadhi waliopo uwandani ili kuongeza ufanisi wa zoezi hilo huku akiwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kulinda wananchi wake na kwamba askari wapo uwandani wanafanya kazi usiku na mchana kuwahakikishia usalama wao.

Nao wananchi wa Simiyu hususani Wilaya ya Itilima wameshukuru juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo, wakisema hatua hiyo imeweza kuwarejeshea matumaini, utulivu na amani.

"Tulikuwa tunasumbuliwa sana na fisi ambao walikuwa wanauma watu, baada ya Serikali kusikia ikaweka ulinzi, kwa kweli imetufanyia vizuri mpaka leo hatujawasikia tena tangu askari waanze kuwashambulia. Tuna utulivu kwa kweli tunashukuru sana," amesema Mozo Mabula mkazi wa Kijiji cha Mwamunhu kilichopo Wilaya ya Itilima.



Powered by Blogger.