NCCR MAGEUZI WAKATAA KUUNGANA NA VYAMA VINGINE UCHAGUZI MKUU

Na Nora Damian, The Page

Chama cha NCCR Mageuzi kimesema hakina mpango wa kushirikiana na chama chochote cha siasa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu na kusisitiza kitasimama chenyewe.

Chama hicho kimesema mwaka 2015 kilijaribu kuungana na vyama vingine na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kudai kuwa hawakupata manufaa kwa kuwa chama chao hakikufaidika kama vyama vingine.

Msimamo huo umetangazwa leo Februari 18,2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti Taifa wa NCCR Mageuzi, Ambari Haji Khamis, alipozungumza na waandishi wa habari.

Mwenyekiti huyo alikuwa akizingumzia chaguzi za ndani za chama hicho na mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Aprili mwaka huu.

"Hatuko kwenye vyama 14 wala sita wala vyama vitatu, sisi tuko peke yetu na tutaendelea kuwa peke yetu mpaka vikao halali vya chama vitakapoona vinginevyo...kwasasa umoja tulishauvunja Dodoma kwenye mkutano mkuu.

"Hatutaki umoja kwa sababu madhara yaliyotukuta 2015 ni makubwa mpaka leo hatujapona. Tuliingia kwenye uchaguzi tukiwa na wabunge wanne tukatoka na mbunge mmoja mengine tukapoteza...sisi hatukufaidika chochote kwenye Ukawa," amesema Khamis.

Mwenyekiti huyo amesema yako maadhimio ambayo walikubaliana na kusaini lakini vyama vingine havikuyatekeleza hivyo hawawezi kurudia makosa.

Aidha amesema kupitia mkutano mkuu utakaofanyika Aprili mwaka huu pia watatangaza jina la mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea urais kwa upande wa Zanzibar pamoja na kupitisha mabadiliko ya katiba ya chama hicho.

Chama hicho kimesema kimejifunza kilipokosea na sasa kimejipanga kuhakikisha kinashiriki vizuri Uchaguzi Mkuu na kushinda kwa kishindo.




Powered by Blogger.