MPOGOLO AONYA WATENDAJI WANAOKWAMISHA WANANCHI MIKOPO YA ASILIMIA 10
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutowakwamisha wananchi wanaohitaji mikopo ambayo inatolewa na halmashauri hiyo kupitia mapato yake ya ndani.
Akizungumza Februari 22,2025 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Kisiwani Kata ya Bonyokwa amesema halmashauri hiyo imetenga Sh bilioni 15 kwa ajili ya kukopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakitengeneza mazingira ya urasimu na kutaka kupewa fedha na waombaji wa mikopo hiyo jambo ambalo linakwamisha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwakomboa wananchi kiuchumi.
"Kuna watumishi hawamuogopi Mungu, vikundi vinapokwenda kuomba msaada wanaambiwa waende steshenari wakapewe mikataba au katiba, wakifika wanatozwa fedha kati ya Sh 150,000 au 200,000.
"Sisi tunalipwa mishahara tuwasaidie wenzetu waweze kupata mikopo. Tumefundishwa namna ya kumsaidia mtu kuingia kwenye mfumo, tumefundishwa namna ya kuandika mchanganuo...huyo aliye steshenari hakufundishwa.
"Niwaombe watendaji tusitengeneze mkwamo, wala tusitengeneze mazingira ya kupata fedha. Mheshimiwa Rais ameleta fedha ili wananchi wanufaike," amesema Mpogolo.
Aidha amewataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutumia vizuri ofisi za Serikali kutatua changamoto za wananchi na kujenga mahusiano mema.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani, Sulela Logeko, amewahamasisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza na kuomba mikopo hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mwenyekiti huyo amesema wamejipanga kutatua kero za wananchi hasa ya ulinzi na usalama kutokana na kuwepo kwa matukio mbalimbali ya watu kuvamiwa hasa nyakati za alfajiri.
Mwenyekiti huyo ambaye alichaguliwa Novemba mwaka jana pia alisoma ripoti ya mapato na matumizi na kuwahakikishia wananchi kuwa atakuwa akihitisha vikao kwa mujibu wa sheria na kuwasomea ripoti hizo ili kurahisisha shughuli za maendeleo katika mtaa huo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo, amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM unakwenda vizuri katika mitaa yote ya kata hiyo na katika bajeti ya mwaka 2025/2026 zimetengwa Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na Sh milioni 70 kuendeleza ujenzi wa kituo cha polisi.
Amesema pia barabara ya Segerea - Bonyokwa yenye urefu wa mita 700 tayari imepata mkandarasi na barabara zingine zitajengwa kupitia mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2) na mitaa yote ya Msingwa, Kisiwani na Bonyokwa itanufaika.
