WAVUVI 540 WAOKOLEWA, 10 WANATAFUTWA ZIWA RUKWA

Na Mwandishi Wetu, Rukwa

Wavuvi 540 waliokuwa wanafanya shughuli za Uvuvi katika Ziwa Rukwa wameokolewa huku wengine 10 wakiendelea kutafutwa.

Tukio hilo limetokea kufuatia upepo mkali uliotokea Januari 23,2025 katika Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amefika katika Kata ya Nankanga kuungana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji, ili kujionea kazi ya uokozi huku akiambata na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, CGF John Masunga pamoja na askari wazamiaji.Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbwanga, Nyakia Chirukile, amesema Januari 23,2025 wavuvi 550 kutoka Kata ya Nankanga na Mtowisa waliokuwa wanaendelea na shughuli za uvuvi katika Ziwa Rukwa walipatwa na dhoruba ya upepo mkali katika ziwa hilo.

Amesema jitihada za kuwaokoa zinaendelea kufanywa na wananchi wakishirikiana na Jeshi la Zimamoto wa Uokoji ambapo hadi kufikia Januari 24,2025 wavuvi 10 walikuwa bado hawajapatikana.

Akitoa salama za pole Waziri Bashungwa amesema Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan baada ya kupata taarifa hizo, ametoa helkopta ya jeshi iliyoambatana na wazamiaji na vifaa maalumu vya uokozi ili kuongeza nguvu za uokoaji. 

Kwa Upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji, amewapongeza wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika uokoaji pamoja na kutoa ushirikiano wa kuwatambua wavuvi wengine ambao walikuwa hawajasajiliwa katika vikundi na makampuni.



Powered by Blogger.